Akina mama wajawazito kujifungulia nchi jirani ya Zambia kutokana na zahanati kuzingilwa na maji ya ziwa Tanganyika

Wakazi wa kijiji cha Kipwa kilichopo mpakani kati ya nchi ya Tanzania na Zambia wameanza kutekeleza agizo la Serikali la kuwataka kuhamia maeneo ya miinuko ndani ya siku 90.

Kijiji cha kipwa kinapatikana kata ya Kasanga wilaya ya Kalambo kando ya ziwa Tanganyika, kutokana na jiografia hiyo kimekuwa kikikabiriwa na ongezeko la maji ya ziwa Tanganyika.

 Hata hivyo mwanzoni mwa mwaka 2021 kijiji hicho kilikumbwa na mafuriko ya maji yaliyokuwa yamesababishwa na kufurika kwa ziwa Tanganyika na kusababisha kaya 209 kukosa makazi na huku baadhi ya wananchi wakilazimika kuishi kwa majirani na sehemu za ibada huku Taasisi za Serikali zikikumbwa na kadhia hiyo.


Licha ya hilo mnamo tarehe 30 Aprili 2021 kamati ya wataalamu wa maafa kutoka Halmashauri ya Kalambo ikiongozwa na kaimu mkurugenzi Ndg. Jabiri Ally ilifika kijijini hapo kwa dhumuni la kujionea adha hiyo na kubaini asilimia 70 ya wakazi wa kijiji hicho kupatwa na adha hiyo,

Kaimu mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Jabiri Ally, alisema nyumba nyingi zikiwemo za watumishi, zahanati na shule ya msingi nazo zimezungukwa na maji na kuathiri utoaji huduma za afya na elimu.


“pia hali ya vyoo kwa sasa sio nzuri jambo ambalo lina hatarisha kutokea kwa janga jingine la mlipuko wa magonjwa kama kipindupindu na uti wa mgongo’’. alisema Jabiri

Hata hivyo kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo ikiongozwa na mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Kalorius Misungwi ilitembelea kijiji hicho na kuamuru  wananchi wote kuhamia maeneo ya miinuko ndani ya miezi mitatu agizo ambalo lilipokelewa kwa shangwe kubwa na  wakazi wa kijiji hicho.


Kamati hiyo pia ilitembelea maeneo ya makazi mapya ya wakazi wa kjiji hicho pamoja na maeneo ya kujenga taasisi za Serikali ikiwemo shule na zahanati.

Awali akiongea na wakazi wa kijiji hicho mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo Mhe. Kalorius Misungwi, alisema kijiji hicho kina jumla ya kaya 357 na kaya 209 zimekosa makazi na kaya 144 ndizo zilizo salia kwa hivi sasa.

Hata hivyo miongoni mwa changamoto kubwa inayowakabiri wakazi wa kijiji hicho katika maeneo mapya ya makazi wanayotarajia kuhamia ni ukosefu wa huduma ya maji pamoja na barabara.


Ziwa Tanganyika lina urefu wa km 673 na upana wa km72 huku eneo lote likiwa na km2 32,900 na ujazo wa km3 18,800 huku urefu wa ufukwe ikiwa ni km 1,828.

 Ziwa Tanganyika limezungukwa na nchi ya Tanzania, Congo, Burundi na Zambia huku wananchi kutoka sehemu zote za nchi hizo wakilitegemea katika shughuli za uvuvi na usafiri.

licha ya uwepo wa ziwa hilo lakini bado kumekuwa na changamoto ya mabadiliko ya tabia ya nchi, ambapo kwa mwaka 2020 /2021 kumekuwa na ongezeko la kupwa na kujaa kwa ziwa hilo hali ambayo imekuwa ikiwasababishia hasara wananchi na Serikali kwa ujumla.

March 30 /2021 kulitokea mabadiliko ya tabia ya nchi ambapo ziwa hilo lilijaa na kufunika kijiji na eneo lenye miundombinu muhimu ya huduma kwa umma. Miongoni mwa miondombinu iliyokumbwa na janga hilo ni viwanda, masoko na makazi ya wananchi likiwemo soko la samaki la Kasanga.

 Hata hivyo adha hiyo imewakumba pia akina mama wajawazito ambao wanalazimika kujifungulia na kupata matibabu katika nchi jirani ya zambia kutokana na zahanati yao kuzingilwa na maji ya ziwa hilo,

kwa nyakati tofauti akina mama kijijini hapo walisema wanalazimika kutumia mitumbwi kusafi  hadi nchi jirani ili kupata matibabu na kwamba changamoto kubwa imekuwa ni watoto ambao wakati mwingine wamekuwa wakizidiwa na kushindwa kupata huduma kwa wakati muafaka.

 

 

Comments