Rais Samia kuzuru Kenya

 

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, atafanya ziara ya kikazi nchini Kenya siku ya Jumanne.

Rais Samia atakuwa katika ziara nchini humo kwa siku mbili ambapo atapokelewa na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta.

Ziara hiyo ya rais Samia ni muendelezo wa jitihada za nchi hizo mbili kuboresha na kuendeleza uhusiano wa muda mrefu na itakuwa ndio ziara ya pili nje ya taifa lake kwa rais Samia tangu alipochukua madaraka kutoka kwa hayati Dkt John Magufuli .

Alifanya safari yake ya kwanza akiwa Rais nchini Uganda mnamo Aprili 11 na Rais Yoweri Museveni akielezea kuwa lengo la ziara yake ni kuimarisha uhusiano wa nchi mbili na kumaliza makubaliano ya mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka nchini Uganda.Uganda na Tanzania zilisaini mikataba mitatu yenye nia ya kuendeleza sekta ya mafuta na gesi ya Uganda, wakati wa ziara ya hiyo.

Akiwa nchini Kenya atafanya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Uhuru Kenyatta kisha atalihutubia Bunge la Kenya litakalojumuisha Wabunge wa Mabunge yote mawili ya nchi hiyo. Taarifa ya Ikulu nchini Tanzania imeeleza.

Aidha, Rais Samia atahudhuria na kuhutubia mkutano wa jukwaa la wafanyabiashara wa Kenya na Tanzania utakaofanyika jijini Nairobi kwa lengo la kujadiliana masuala yahusuyo fursa za kibiashara na uwekezaji zilizopo nchini Tanzania na Kenya kwa mujibu wa taarifa iliyotumw ana kurugunzi ya mawasiliano ya Ikulu

Rais Samia amedhihirisha si mara moja kuhusu nia yake ya kuvutia wawekezaji kwenda Tanzania . Ziara hii yake nchini Kenya itakuwa mojawao ya jitihada za kuwahakikishia mazingira bora wawekezaji walioko nchini Kenya kufungua biashara zao nchini humo.

 

Kulikuwepo awali na changamoto kwa wawekezaji hasa kutoka mataifa ya kigeni kuendeleza shughuli zao za kibiashara nchini Tanzania na hilo rais Samia alilitaja hata katika hotuba yake kwa bunge la Tanzania alipoeleza umuhimu wa serikalia kuhakikisha kwamba wawekezaji wanapata urahisi wa kuendesha shughuli zao nchini mwake

 

Comments