Na Baraka Lusajo - Kalambo.
Serikali katika
lengo lake la kumtua mama ndoo kichwani, imetoa fedha kiasi cha shilingi
milioni 402 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji ambayo inatarajiwa
kuhudumia vijiji 11 vyenye zaidi ya wananchi elfu sita (6000) katika
Halmashauri ya wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa na kuwaondolea adha wananchi
kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo katika mto Mzwalo.
Meneja wa RUWASA
wilayani Kalambo Patrick Ndimbo, amesema mradi wa Singiwe ulianza kutekelezwa Julay
25/2020 na makadirio ya mradi ilikuwa ni shilingi 416,891,454 na kutakiwa
kutekelezwa kwa muda wa miezi mitatu.
‘’Kabla ya ujenzi
wa mradi huu hapakuwa na huduma ya uhakika ya maji, kwa kuwa mradi uliokuwepo
ulikuwa wa miaka mingi na miundomdombinu yake ilikuwa chakavu sana. Pia kazi
zilizofanyika katika mradi huu mpya ni sawa na asilimia 50% na mpaka sasa
tumetumia fedha kiasi cha shilingi million 170,524,282 sawa na asilimia 41% ya
makadirio ya mradi wote.
Mkuu wa TAKUKURU wilayani
humo Lupakisyo Mwakyolile, amesema mradi huo wanaufuatilia kwa ukaribu lengo likiwa
ni kuhakikisha unakamilika kwa wakati na
kuwawezesha wananchi kunufaika na huduma hiyo muhimu.
Akiongea mara
baada ya kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo kutembelea na kukagua mradi
huo, mkuu wa wilaya hiyo Calorus Misungwi, amesema ujenzi wa miradi hiyo
itawawezesha kupata maji safi na salama kwa wakati wote na kuwasihi watumiaji
wa maji kulinda miradi hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu.
Ili kuwa na miradi
endelevu ya RUWASA wilaya ya Kalambo kwa
kushirikiana na ofisi ya Mkurugenzi mtendaji
kupitia idara ya maji (CBWSO) inayojulikana kwa jina la Jumuhiya ya watumiaji
maji Mzwalo ambayo itasimamia uendeshaji wa matengenezo ya mradi wa maji
Singiwe pindi ukikamilika.
Comments
Post a Comment