Halmashauri ya Kalambo mkoani Rukwa imeanzisha kampeni ya utoaji elimu kwa wananchi wanaoishi kando ya mito na maeneo ya wazi ili kuchukua tahadhari kwa kupanda miti sambamba na kuyahama maeneo hatarishi.
Kampeni hiyo imeongozwa na afisa maafa wilayani humo Mejoni Ndenje na kufanyika katika kijiji cha Chalaminwe kata ya Lyowa wilayani humo na kusisitiza jamii kujenga nyumba bora na vyenye uwezo wa kuhimili vishindo vya mvua na upepo kipindi cha mvua za masika.
Afisa mazingira wilayani humo Julieth Tarimo aliwataka wananchi wilayani humo kuacha kuendesha shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo na ufugaji kwenye vyanzo vya maji, kupanda miti rafiki kwenye vyanzo vya maji, kuepuka kuchoma moto kwenye misitu na kusimamia sheria ndogo za mazingira, kwa lengo la kutunza na kuhifadhi mazingira.
‘’kwa kuzingatia sheria ya mazingira namba 20 ya mwaka 2004 kifungu cha 57(1) na kifungu cha (2) ndani ya mita 60 hakutafanyika shughuli yoyote ya binadamu ya kudumu au ambayo kwa asili yake inaweza kuhatarisha au kuathiri vibaya ulinzi wa mazingira.Kwa yeyote atakayekiuka atachukuliwa sheria kulingana na sheria ndogo za mazingira’’Alisema Tarimo.
Diwani wa kata hiyo Benard Mwamsojo aliwataka wazazi na walezi kwenye maeneo hayo kuwalinda watoto wao hususani kipindi cha mvua ili kuwaepusha na adha ya kusombwa na maji ya mvua.
Comments
Post a Comment