Wanafunzi Elimu Ya Awali Kupewa Kipaumbele Mkoani Rukwa

 


Baraka Lusajo – Rukwa

Programu ya Serikali kupitia ya Shule Bora imedhamiria kuwezesha walimu na wasimamizi wa elimu kubainisha changamoto na fursa katika ufundishaji na ujifunzaji wa stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK) kwa madarasa ya awali,la kwanza na la pili ili kuepusha watoto kumaliza darasa la saba bila umahili .

Shule Bora ni programu ya elimu inayolenga kuinua ubora wa elimu jumuishi inayotolewa kwenye mazingira salama ya kujifunzia kwa wasichana na wavulana kwenye shule za umma nchini Tanzania na inafadhiliwa na Shirika la Misaada la Uingereza (UKAID) kutoka Serikali ya Uingereza.

Akifungua mafunzo ya usimamizi wa ufundishaji wa KKK katika shule za msingi kwa maafisa elimu mkoa na wilaya , Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Rashid Mchatta kupitia hotuba yake iliyosomwa na Afisa Elimu Mkoa huo Samson Hango Februari katika mji wa Namanyere Nkasi alisema tatizo la watoto kutojua kusoma na kuandika bado lipo.

“Takwimu zinaonesha kuwa hadi Desemba 2022 zaidi ya wanafunzi 25,000 kuanzia darasa la kwanza hadi la saba hawamudu stadi za KKK kwa mkoa mzima wa Rukwa. Hali hii ni hatari kwa maendeleo ya mkoa na taifa” alisema Mchatta.

Kupitia mafunzo hayo ya siku tano walimu na maafisa elimu toka halmashauri nne za Sumbawanga Manispaa, Sumbawanga Vijijini, Nkasi na Kalambo watajengewa uwezo toka wataalam toka Taasisi ya Elimu Tanzania (TEA), OR-Tamisemi ,Shule Bora na Wizara ya Elimu kuhusu namna ya kuwasaidia kupata umahiri wa ufundishaji KKK .

Kwa upande wake Mratibu wa Mafunzo hayo toka Taasisi ya Elimu Tanzania (TEA) Mwesiga Kabigumila alisema tatizo la wanafunzi kutomudu stadi za KKK linachangiwa na baadhi ya walimu kukosa mbinu za ziada za kufundisha watoto wa madarasa ya awali na la kwanza .

Mwesiga alisema programu hiyo inakwenda kuwafikia walimu wa shule Arobaini (40) za mkoa wa Rukwa wanaofundisha madarasa ya awali ,la kwanza na la pili ili wapate mbinu na stadi za kwenda kusaidia wenzao shuleni.

“Katika mafunzo haya walimu na wasimamizi wa ngazi ya halmashauri watapata mbinu mbalimbali ili kuinua ari ya watoto kupenda shule na kumudu kufundisha madarasa makubwa katika mazingira ya sasa “ alisema Mwesiga.

Naye Mwezeshaji mafunzo toka chuo cha ualimu Nachingwea Omar Patrick alisema katika mafunzo hayo walimu watafundishwa namna bora na rahisi ya kutayarisha zana za kufundishia watoto wa awali na darasa la wkanza ili wapende kusoma .

Nao Maafisa Elimu toka Sumbawanga Manispaaa na Sumbawanga vijijini Patricia James na Mery Kaisi walisema watatumia mafunzo hayo kuwesa kusimamia kwa karibu ufundishwaji wa wanafunz wakiwemo wale wenye mahitaji maalum kwani mradi wa Shule Bora unalengo hilo pia.

Programu ya Shule Bora inayotekeleza vipaumbele vya mpango wa Taifa wa Maendeleo wa sektaya elimu (ESDP) katika mkoa wa Rukwa inatekelezwa katika halmashauri nne , shule za msingi za serikali 382 na vituo kumi na saba (17) vya majaribio ya utayari kwa kuanza shule katika kata nane (8) za majaribio katika mwaka huu wa kwanza ambapo mradi unatarajia kufikia ukomo mwaka 2027.

 

Comments