Maadhimisho Ya Wiki Ya Lishe Vijijini Yajikite Kuhamasisha Jamii Kutoa Lishe Bora Kwa Watoto


Na Baraka Lusajo – Rukwa

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga ameelekeza halmashauri zote mkoani humo kuandaa maadhimisho ya wiki ya utoaji elimu ya lishe bora katika ngazi za vijiji ili kukabiliana na tatizo la udumavu.

Ametoa kauli hiyo  mjini Sumbawanga wakati wa hafla ya kukabidhi pikipiki Kumi na Mbili (12) kwa maafisa lishe wa halmashauri zilizotolewa na serikali kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la udumavu ambao kwa Rukwa upo asilimia 47.9 kwa takwimu za mwaka 2018.

Sendiga alibainisha kuwa maadhimisho hayo yakifanyika itakuwa jukwaa zuri la wataalam wa lishe kutoa elimu ya uandaaji vyakula bora na ulaji sahihi kwa kutumia vyakula vinavyopatikana kwenye mazingira ya Rukwa kwa kuwa mkoa huo ni mzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula na kuifikia jamii kwa wakati ili watoto waweze kupata lishe bora

Akitoa taarifa ya vifaa hivyo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Ibrahim Isaack alisema jumla ya pikipiki Kumi na Mbili zimetolewa kwa Halmashauri za Kalambo (4), Sumbawanga Vijijini (3), Nkasi (3) na Manispaa ya Sumbawanga (2).

Dkt. Ibrahim alisema pikipiki hizo zitakwenda kufanya kazi ya elimu ya lishe, kuboresha utoaji chanjo  kwa watoto wenye umri chini ya miaka 5 na kufuatilia magonjwa ya milipuko vijijini.

Mwisho.

Comments