Wananchi Wilayani Kalambo Wahimizwa Kuchanja Mbwa Na Paka Ili Kuepuka Kichaa Cha Mifugo Hiyo.

Na IO - Kalambo 

Wananchi wilayani Kalambo mkoani Rukwa wameungana na watu wengine duniani katika kuadhimisha kumbukumbu ya kichaa cha mbwa huku Halmashauri kwa kipindi cha wiki moja ikifanikiwa kutoa chanjo kwa mbwa 300.


Halmashauri ya wilaya ya Kalambo ina jumla ya mbwa 6,714 na paka 1,178 ambapo katika kipindi cha mwaka 2020/2021 mbwa wapatao 215 walichanjwa na kwa mwaka 2021 /2021 mbwa 525 na paka 2 walipata chanjo huku kwa mwaka 2022 / 2023 mbwa wapatao 724 na paka 13 wamepatiwa chanjo.

Hata hivyo maadhimisho ya kumbukumbu ya kichaa cha mbwa hufanyika september 28 ya kila mwaka ambapo kwa mwaka 2022 maadhimisho hayo yamefanyika kikanda katika eneo la kateka kata ya Matai wilayani humo yakiwa na lengo la kuhamasisha jamii kuchanja mbwa na paka.

Mapema akiongea wakati maadhimisho hayo mganga mkuu wa mifugo wilayani Kalambo Enossy Luvinga amesema kichaa cha mbwa ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vya kichaa cha mbwa na huathiri wanyama wote ikiwemo mbwa na binadamu


Alisema ugonjwa huo hauna tiba na kwamba unaweza kukingwa kupitia chanjo ikiwa ni pamoja na kuzingatia ufugaji bora wa mbwa na paka.

Awali akiongea kupitia maadhimisho hayo mkuu wa wilaya hiyo Tano Mwela akawataka wananchi kuhakikisha mifugo yao inapata chanjo.

‘’Serikali imetengeneza kanuni za chanjo na uchanjaji ya mwaka 2020 ambazo zinalazimisha kila mfugaji kuchanja mbwa na mifugo mingine dhidi ya magonjwa mbalimbali hivyo basi wafugaji wote kwa umoja wenu mnasisitizwa pindi mtakaposikia uwepo wa shughuli za uchanjaji wa mifugo mnapaswa kushiriki kikamilifu’’ Alisema Mwela.

Comments