Wananchi Katika Kijiji Cha Singiwe Waazimia Kuchukua Hatua Dhidi Ya Wazazi Walioshindwa Kutoa Malezi Kwa Watoto Wao.



Na Baraka Lusajo- Rukwa

Wananchi katika Kijiji cha Singiwe kata ya Lyowa wilayani Kalambo mkoani Rukwa wameazimia kuchukua hatua kali dhidi ya wazazi na walezi ambao watabainika kushindwa kudhibiti uzurulaji wa watoto wao nyakati za usiku.

Hatua hiyo inakuja baada ya kujitokeza wimbi la watoto kuanzia miaka 3-8 kukutwa mitaani nyakati za usiku wakizurula na wengine kukutwa kwenye kumbi za kuoneshea video huku wazazi wao wakionekana kutokuwa na habari na familia zao.


 Akiongea kupitia mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo,Mwenyekiti wa kijiji cha Singiwe  Donard Songolo , alisema kwa kutambua umuhimu wa ulinzi wa watoto wameanza kuchukua hatua dhidi ya wazazi ambao wamekuwa wakishindwa kuwadhibiti watoto wao nyakati za usiku na kuishia kuangalia video kwenye mabanda umiza huku wengine wakilazimika kulala kwa majirani kutokana na ukosefu wa uangalizi.

‘’tunataka wazazi wawe waangalizi na walinzi wa watoto wao hivyo mzazi au mlezi ambae ataonekana kushindwa kumlea mtoto wake atachukuliwa hatua kali za kisheria kwani tumeshuhudia kila siku watoto  hususani kuanzia miaka 3 wanakuwa kwenye sehemu za kuoneshea video muda ambao walipaswa kuwa nyumbani hali ambayo ni hatari. Alisema chongolo

Diwani wa vitimaalmu katika tarafa ya,Matai wilayani humo  Yuster Kajema , alisema lengo la serikali ni kuhakikisha watoto wote wanalindwa ikiwemo kutambua haki zao za msingi , kupatiwa elimu , malazi na mavazi na kwamba kwa kufanya hivyo ndivyo itaonekana kweli tunawalinda.

‘’lengo la serikali ni kuhahakikisha huduma za malezi jumuishi ya watoto zinawafikia watoto wote wenye umri kuanzia miaka (0-8) pamoja na kuzingatia masuala ya jinsia, watoto walio katika mazingira hatarishi kwa mfano watoto wote wenye VVU, Yatima ,watoto wanao umwa sana pamoja na wenye utapia-mlo ,watoto walipo mahabusu ,kambini na wenye changamoto katika ukuaji  wote kwa umoja wao wanapaswa kulindwa na kupata stahiki muhimu.’’alisema Kajema.

Hata hivyo katika kuhakikisha haki za watoto zinatambulika na kutekelezwa, Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoridhia na kusaini mkataba wa kimataifa wa haki za mtoto na mapendekezo ya kamati Na. 7 ya mwaka 2005 katika kutekeleza haki za watoto.

 

Comments