TANROADS RUKWA YAFANIKISHA UJENZI WA MADARAJA 13

Serikali ya Awamu ya Sita katika kipindi chake cha mwaka mmoja tangu kuingia madarakani kupitia Wakala wa Barabara (TANROADs) umefanikiwa kutekeleza kazi za matengenezo ya dharura ikiwemo madaraja 13 katika barabara za mkoa wa Rukwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana wakati wa ukaguzi wa barabara katika kijiji cha Muze kilichopo katika Bonde la Ziwa Rukwa Wilaya  Su
mbawanga (22 Machi,2022) Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Rukwa Mhandisi Mgeni Mwanga alisema Serikali ilitoa shilingi 13,864,528,000/- katika mwaka wa fedha 2021/22.

 Mafanikio hayo yamekuja ikiwa ni jitihada za serikali kufanya matengenezo ya dharura katika barabara za Rukwa ikiwemo ile ya Kasansa –Muze –Kilyamatundu iliyopo ukanda wa Ziwa Rukwa yenye urefu wa kilometa 179 ambayo iko chini ya Wakala wa Barabara (TANROAD) hatua iliyofanya ipitike bila shida kipindi chote cha mwaka.

“Rais Samia Suluhu Hassan amefanikisha upatikanaji wa fedha katika bajeti ya mwaka 2021/22 kwa ajili ya matengenezo ya dharura ya miundombinu ya barabara ambapo tulifanikiwa kujenga madaraja 13 katika barabara za mkoa wa Rukwa” alisema Mhandisi Mgeni.

Mhandisi Mgeni aliongeza kusema miradi hiyo ya ujenzi imefanyika kwa kutumia wakandarasi wazawa hatua inayosaidia kukuza uchumi wa mkoa na Taifa.

Katika hatua nyingine TANROAD imesema serikali iko katika mpango wa ujenzi wa barabara ya Ntendo –Kazungu yenye  umbali wa kilometa 25 na barabara ya Kazungu –Muze  yenye urefu  wa kilometa   12 kwa kiwango cha lami ambapo ujenzi utaanza mwaka wa fedha 2022/23.

Akizungumzia umuhimu wa barabara  ya ukanda wa Ziwa Rukwa Diwani wa Kata ya Zimba tarafa ya Mtowisa ,Ephraim Konta alisema kukamilika kwa miundombinu ya ikiwemo daraja la Lwanji kumesaidia kurahisisha shughuli za kiuchumi kwani mazao yanafika sokoni yakiwa katika ubora .

Diwani huyo aliongeza kusema anaomba serikali kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kutofanya shughuli za kilimo na Mifugo katika kingo za mito hatua itakayosaidia madaraja kuwa imara na mito kutokana hama.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Solola halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga, Godfrey Tanganyika alishukuru serikali kwa kujenga daraja lililokuwa kikwazo cha kuunganisha kijiji hicho na kijiji cha Ilemba kufuatia mvua kusababisha mto kuhama.

“Tunashukuru serikali kwa kujenga daraja hili pia tunamwomba Rais Samia atuwekee lami katika barabara hii ya ukanda wa Ziwa Rukwa kwani ndio barabara kubwa iliyobaki bila lami” alisema Tanganyika.

Nao wanafunzi Felista Zuberi na Elizabeth Nasri wa kidato cha nne shule ya sekondari Mazoka iliyopo kata ya Muze walisema kukamilika kwa ujenzi wa daraja la Muze kumesaidia waweze kuwa na uhakika wa kuhudhuria masomo muda wote ikiwemo kipindi cha masika.

“Tulikuwa tukikosa masomo kipindi mto huu ulipokuwa ukijaa na njia kukatika kwani tunaishi Muze na shule iko upande wa pili kijiji cha Mazoka kata ya Mbwilo” alisema Felista mwenye umri wa miaka 18.

Wakala wa Barabara (TANROAD) Mkoa wa Rukwa unaendelea na kazi ya kusimamia mtandao wa barabara Kuu za lami zenye urefu wa kilometa 415 .86 kati yake za lami kilometa 298.35 na za changarawe kilometa 117  huku ikisimamia barabara za mkoa zenye urefu wa kilometa 834.98 kati ya hizo za lami ni kilometa 76.83 na za changarawe ni kilometa 758.15

 

Mwisho


Comments