Ruwasa Yatumia Bilioni 16 Kukamilisha Miradi 39 Ya Maji Rukwa


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti amepongeza Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Rukwa kwa kufanikiwa kutekeleza miradi 39 ya maji yenye gharama ya shilingi Bilioni 16.6 katika mwaka wa fedha 2021/2022 kwenye mkoa wa Rukwa ikiwa ni juhudi za kumtua mama ndoo kichwani.

Mkirikiti amesema hayo leo (11 Aprili 2022) mjini Sumbawanga wakati akiongea kikao cha wadau wa maji ulioratibiwa na RUWASA mkoani huo ukiwa na lengo la kuwafahamisha wadau hatua zilizofikiwa kwenye utekelezaji bajeti na mipango ya kufikisha huduma za maji vijijini.


 Mkuu huyo wa Mkoa alitaja mafanikio mengine ya RUWASA kuwa ni pamoja na huduma za upatikanaji maji kuongezeka kufikia asilimia 64 vijijini na mjini imefikia asilimia 86 kutokana na kukamilika kwa miradi hiyo 39 kati ya miradi 99 yenye thamni ya shilingi Bilioni 25.5 iliyosainiwa mwaka 2021/22 .

“Niwapongeze RUWASA kwa usimamizi mzuri wa miradi hii ya maji, hatua hii inasaidia wananchi kupata maji safi na salama na kuboresha afya hivyo kuwafanya wananchi waendelee kushiriki vema kwenye utekelezaji shughuli za maendeleo” alisema Mkirikiti

Mkirikiti alibainisha kuwa pamoja na jitihada za serikali kutoa fedha kwa miradi ya maji bado kuna changamoto ya uharibifu wa mazingira hususan vyanzo vya maji ikiwemo shughuli za kilimo ndani ya mita Sitini ya maziwa, mito na mabwawa .

“ Kama kuna fedha imeletwa lazima uhakikishe mradi huo unakamilika , hilo ndio lengo la Rais Samia Suluhu Hassan . Katika hili sihitaji kuona hadithi toka kwa watendaji ndani ya Rukwa” alisisitiza Mkirikiti.

Kwa upande wake Meneja wa RUWASA Mkoa wa Rukwa Mhandisi Boaz Pius alisema lengo la kikao hicho ni kuwaeleza wadau kuhusu juhudi zinazofanya na Wizara ya Maji katika kuondoa kero ya ukosefu wa maji  vijijini.

Mhandisi Boaz aliongeza kusema RUWASA inaandaa mikakati kwa kuunganisha vyombo vya watumie maji kote vijijini ili kuwa na vyombo vichache venye wataalam waliobobea ili wasimamie utoaji huduma badala ya kuwa na idadi kubwa ya vyombo hatua inayoongeza gharama za uendeshaji.

Akitoa mada kuhusu michango wa Vyombo vya Watumia Maji ngazi ya Jamii (CBWSOS) Afisa Maendeleo ya Jamii RUWASA Nanyari Lona alisema kiasi cha shilingi 168,423,720 zimekusanywa na vyombo ambapo kati ya hizo shilingi 127,033,162 zilirudishwa kwenda kuendesha vyombo na matengenezo ya miundombinu ya maji.

Comments