Kalambo yaazimisha miaka 58 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibari kwa kufanya usafi wa mazingira.



Halmashauri ya wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa imeazimisha miaka 58 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kufanya usafi kuzunguka maeneo ya hospitali ya wilaya hiyo huku wananchi wilayani humo wakihimizwa kulifanya zoezi hilo kuwa endevu kwa kufanya usafi kila siku badala ya kusubiri matukio ya kitaifa kwa lengo la kufanya mazingira kuwa safi muda na wakati wote.

Wakiongea wakati wa shughuli za usafi wa mazingira kuzunguka maeneo ya hospitali ya wilaya hiyo kama sehemu ya kuazimisha miaka 58 ya muungano, viongozi wa serikali wilayani humo wamesema zoezi hilo linapaswa kuwa endelevu.


Akiongea wakati wa shughuli za usafi wa mazingira, mkuu wa wilaya hiyo Tano Mwela, alisema wameazimisha miaka 58 ya muungano wa Tanganyika kwa kufanya usafi kuzunguka hospitali ya wilaya hiyo kama njia ya kuhamasisha jamii kujenga mazoea ya kufanya usafi kila siku na kuwataka wananchi kujenga mazoea ya kufanya usafi kila wakati pindi wanapopata nafasi ili kuyafanya mazingira kuwa bora na salama.


Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo Shafi Mpenda,alisema swala la usafi ni maelekezo ya serikali ambayo yanawataka wananchi  na watumishi wa umma kufanya usafi kila mwezi  kuzunguka maeneo yao husika na kwamba wameazimisha miaka 58 kwa kufanya usafi katika maeneo hayo kama njia ya kuunga mkono jitihada za serikali  juu ya uwekezaji wa hospitali hiyo.

 ‘’Kikubwa sisi kama watumishi wa umma tunachokifanya ni kuwakumbusha wananchi kwamba kila mwezi lazima tufanye usafi hivyo kikubwa wananchi lazima elimu hii iwaingie ili kujua kuwa usafi ni jukumu la kila mmoja.’’ alisema Mpenda.


Hata hivyo Halmashauri mbalimbali mkoani Rukwa zimeazimisha miaka 58 ya muungano kwa kufanya shughuli tofauti, ambapo watumishi kupitia ofisi ya mkuu wa mkoa wa Rukwa imeazimisha miaka 58 kwa kufanya usafi wa mzingira kuzunguka maeneo yote ya ofisi ya mkuu wa mkoa wa Rukwa.

Mkirikiti ameshiriki zoezi hilo la usafi (26.04.2022) katika maeneo ya Ofisi yake zilizopo mjini Sumbawanga huku akisisitiza  watanzania kueendelea kuwa wamoja na wenye kuheshimiana hatua inayokuza utaifa.

“Leo ni siku muhimu kuona kama watumishi tukiwa na umoja na upendo kati yetu wa Bara na wenzetu wa Zanzibar kufuatia uwepo wa Muungano wa nchi zetu mbili. Tuuenzi Muungano wetu huu ili udumu kwa vizazi vingi zaidi vijavyo” alisisitiza Mkirikiti.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Donald Nssoko aliwapongeza watumishi wa umma waliopo makao makuu pamoja na taasisi zilizopo kwenye jengo la mkoa kwa kujitokeza kuadhimisha sherehe za Miaka 58 ya Muungano kwa kufanya Usafi hatua inayoongoza ushirikiano miongoni mwa watumishi hao.

Nae Dkt. Uwezo Kinahi akizungumzia kwa niaba ya watumishi alieleza kuwa tukio hilo alisema anawapongeza watanzania kwa kudumisha Muungano na kuwa kitendo cha kufanya usafi siku ya leo ni mwendelezo wa kuonesha umoja wa watanzania mahala pa kazi.

Dkt. Kinahi amewasihi wananchi wa Rukwa kuendeleza mshikamano wa kidugu na wananchi wa Zanzibar ili kwa pamoja Tanzania ipige hatua zaidi ya kimaendeleo.

Watanzania leo wanaadhimisha sherehe za miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Comments