Halmashauri Ya Kalambo mkoani Rukwa Yafikia 95.9 % Ya lengo la Utekelezaji Wa Opresheni Ya Anuani Na Makazi

 


Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew ameupongeza mkoa wa Rukwa kwa kazi nzuri ya utekelezaji operesheni ya anwani za makazi ambapo hadi kufikia leo imefikia asilimia 97 ya lengo.

Mhandisi Kundo ametoa pongezi hizo  leo (27.04.2022) wakati wa kikao kazi na viongozi na watendaji wa wilaya , halmashauri na taasisi za umma wa mkoa wa Rukwa kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Sumbawanga .

“Hadi kufikia tarehe 26 Aprili 2022 mkoa wa Rukwa umefanikiwa kutekeleza zoezi la anwani za makazi na uwekaji Postikodi kwa kiwango cha asilimia 97 na kushika nafasi ya 24 kwa mikoa ya Tanzania Bara. Niwapongeze viongozi wote mkiongozwa na Mkuu wa Mkoa Joseph Mkirikiti kwa kazi nzuri” alisema Naibu Waziri Mhandisi Kundo.


Naibu Waziri huyo aliongeza kusema ameridhishwa na namna operesheni hiyo ilivyotekelezwa kwenye halmashauri za mkoa wa  Rukwa na kuwa amepita katika mitaa ya Manispaa ya Sumbawanga na kuona kazi kubwa na nzuri iliyofanyika.

Mhandisi Kundo alisema “lengo kubwa ni kufikia malengo tuliyojiwekea kama mkoa na Taifa. Nawapongeza Wakurugenzi wote wa Halmashauri kwa hatua iliyofikiwa kwenye zoezi hili” na kuongeza waendelee kukamilisha kazi zilizobaki kwa weledi na ubora zaidi.

“Nimepita mikoa mingi, lakini hapa Sumbawanga Manispaa nimezunguka kwenye mitaa na kuongea na vijana waliofanikiwa kupata ajira kupitia zoezi hili na kuridhika namna linavyotekelezwa. Hongereni mkoa wa Rukwa kwa kutekeleza maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan” Naibu Waziri Kundo alipohitimisha hotuba yake.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri huyo wa Habari ameziagiza TANROAD na TARURA kushiriki kikamilifu katika kutekeleza agizo la Waziri Mkuu la kuweka anwani na vibao kwenye barabara wanazozisimamia badala ya kusubiri fedha za halmashauri.

Akitoa taarifa ya Mkoa kuhusu utekelezaji wa operesheni anwani za makazi Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Donald Nssoko alisema malengo ni kutambua jumla ya barabara 7,295 na anwani za makazi zipatazo 238,206 ambapo hadi jana imefikia asilimia 98 ya usajili wa anwani.

Nssoko alitaja halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kuongeza kwa kufanya vizuri kwa asilimia 106 ikifuatiwa na Nkasi (96.4 ), Kalambo ( 95.9) na Sumbawanga Manispaa ( 90.3) na kuwa zoezi litakamilika ifikapo Aprili 30 mwaka huu ambapo changamoto zinaendelea kutatuliwa..

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa huo Joseph Mkirikiti alimweleza Naibu Waziri huyo wa habari kuwa mkoa wa Rukwa utakamilisha zoezi bila kumuumiza yeyote kwa kuwa kila mmoja anatimiza majukumu yake kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa.

Mkirikiti aliongeza kusema watendaji ndani ya halmashauri wameelekezwa kuzingatia mwongozo wa operesheni hii ili malengo ya serikali ikiwemo Ilani ya Uchaguzi ya CCM yatimie.

Akizungumza kwa niaba ya viongozi wa dini Askofu Ambele Mwaipopo wa Kanisa la KKKT Dayosisi ya Ziwa Tanganyika alisema ushirikiano uliooneshwa kwenye operesheni hii uendelezwe ili mji wa Sumbawanga upangike na kuvutia.

“Sumbawanga yetu ila utamaduni mitaa inajulikana hakuna makazo holela. Niombe Mamlaka kudhibiti watu wachache wabinafsi kutumia fedha zao kuharibu mipango miji kwa ujenzi usiofuata sheria ili zoezi hili la Postikodi liwe na manufaa kwa taifa” alisisitiza Askofu Mwaipopo.

Naibu Waziri Kundo amekamilisha ziara yake ya siku moja mkoani Rukwa ya kukagua operesheni ya anwani za makazi iliyoanza kutekelezwa mwezi Februari mwaka huu na kueleza kuwa zoezi litakamilika mwezi Mei mwaka huu.

Comments