Watoto chini ya miaka 8 walindwe dhidi ya vitendo vya ukatili.

 

Na Baraka Lusajo – Rukwa.

Wanawake wilayani Kalambo mkoani Rukwa wamesema kuna umuhimu wa serikali kuangalia namna bora ya kudhibiti vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto ambavyo wakati mwingine vimekuwa vikijitokeza katika jamii na kuathiri makuzi na maendeleo ya awali   ya watoto hususani wenye umri chini ya miaka 8

Waliyabainisha hayo kupitia maadhimisho ya uzinduzi wa jukwaa la uwezeshwaji kiuchumi la wanawake yaliyofanyika katika kata ya Matai wilayani Kalambo mkoani Rukwa na kusema vitendo vya ukatili wa kijinsia wakati mwingine vimekuwa vikiwaathiri zaidi akina mama wajawazito ambao wamekuwa wakikumbana na ukatili wa aina tofauti ikiwemo vipigo na kusababisha wengine kupoteza viumbe tumbo.


Akiongea kupitia uzinduzi wa jukwaa la uwezeshwaji kiuchumi la wanawake wilayani humo, mwenyekiti wa jukwaa hilo Ester Msigwa, alisema wanawake wajawazito ni miongoni mwa watu ambao wamekuwa wakikabiliwa na matukio ya ukatili ambao wakati mwingine umekuwa ukiathiri kuhudhuria huduma za afya kama huduma za mama mjamzito.

‘’Pia wanawake wajawazito wameripotiwa kupitia aina tofauti za unyanyasaji ambapo kati asilimia 7 mpaka 10 wametajwa kupitia ukatili wa kijinsia ukiathiri kushindwa kuhudhuria huduma za afya kama huduma ya mama mjamzito, Sambamba na kiwango kikubwa cha ukatili wa kimwili dhidi ya wanawake kimekuwa kikiripotiwa hivyo kuna umuhimu wa serikali Kushirikiana na majukwaa haya ili kusaidia katika utoaji elimu.’’ Alisema Msigwa.


Kaimu afisa maendeleo ya jamii anayeshughulika na makundi ya wanawake,vijana na watu wenye hali ya ulemavu Yasina Nkyabonaki, alisema kwa kutambua umuhimu wa makundi hayo Halmashauri imetoa fedha kiasi cha shilingi million hamsini ili kusaidia makundi hayo kujikwamua kiuchumi.

Alisema,wanawake wakiwezeshwa watakuwa na uwezo wa kulea familia zao na kuondokana na hali ya ukali ambao wakati mwingine umekuwa ukifanyika  pengine kutokana na manyanyaso kutoka kwenye koo au familia zao husika.

Awali akizungumza na hadhara ya wanawake kupitia maadhimisho hayo mkuu wa wilaya hiyo Tano Mwela, alisisistiza wananchi kujiepusha na vitendo vya ukatili kwa kuchukua hatua na kutoa taarifa za uwepo wa matukio hayo kwenye maeneo yao husika ili serikali iweze kuchukua hatua.

Alisema familia zinapaswa kuwekeza katika malezi ya watoto kwa kuhakikisha wanapata huduma na malezi bora ambayo yatawezesha kuongeza kasi ya mafanikio katika malezi na makuzi ya awali ya watoto na hatimaye kufikia ukuaji timilifu.

Hata hivyo kwa mujibu wa takwimu za taifa za makisio ya idadi ya watu zilizotolewa na idara ya afya Takwimu ya Taifa.Tanzania ina takribani ya watoto 16,524,201 wavulana wakiwa 8,328,142, na wasichana 8,196,056 wenye umri kuanzia 0 -8 ambao ni 30% ya watu wote .

Comments