Watoto 36,640 wa andikishwa kujiunga na masomo ya awali mkoani Rukwa



Na Barala Lusajo – RUKWA

Mkoa wa Rukwa umefanikiwa kuwezesha wanafunzi 16,264 waliochaguliwa kuanza kidato cha kwanza mwaka 2022 kuripoti shuleni kati ya lengo la wanafunzi 20,324 waliochaguliwa baada ya kufaulu mtihani wa darasa la saba mwaka jana.

Akizungumza katika ufunguzi wa kikao cha wadau wa elimu leo (24.02.2022) mjini Sumbawanga, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti alisema mafanikio hayo yametokana na jitihada za serikali ya Awamu ya Sita kufanikisha ujenzi wa madarasa 259 katika shule za sekondari chini ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19.

“Wanafunzi wa kidato cha kwanza walioripoti hadi kufikia tarehe 22 Februari, 2022 ni 16,264 sawa na asilimia 80.2 ya wanafunzi 20,324 waliochaguliwa. Na uandikishwaji wa wanafunzi wa darasa la elimu ya awali umefikia asimilia 90.4 baada ya wanafunzi 36,640 kuandikishwa kati ya wanafunzi 42,702 waliotarajiwa katika mkoa wa Rukwa” alisema Mkirikiti.

Mkirikiti aliwataka wadau hao wa elimu kuweka mikakati ya kujua watoto 4,060 ambapo hawajaripoti kidato cha kwanza wako wapi kwani serikali imeweka mazingira mazuri ikiwemo utoaji elimu bila malipo kwa elimu msingi.

Mkirikiti alitoa agizo kwa wadau wa elimu kufanya kazi ya kujua wanafunzi wenye mahitaji maalum walipo na ikiwemo sababu gani wengine hawajaandikishwa shuleni pia wakuu wa shule za sekondari za bweni kusimamia nidhamu za wanafunzi.

“Natoa wito kwa wakuu wa shule zenye hosteli wa mabweni kudhibiti mienendo na maadili ya watoto .Zipo dalili kuwa baadhi mienendo yao siyo mizuri” alionya Mkirikiti.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa mkoa alitoa pongezi kwa serikali ya awamu ya sita kwa kuupatia mkoa huo shilingi Bilioni 6.6 chini ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO-19 zilizotumika kujenga vyumba vya madarasa 259 shule za sekondari na madarasa 73 kwa vituo shikizi vya shule za msingi.

“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha zilizowesha kujengwa miundombinu ya madarasa mapya yaliyowezesha wanafunzi wote waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza mwaka huu 2022 kuripoti vema shuleni” alisisitiza Mkirikiti.

Naye Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu akizungumza kwenye kikao hicho cha wadau wa elimu alisema lengo lake ni kufanya tathmini ya hali ya elimu kwa kuangalia mafanikio yaliyopatikana na namna ya kuboresha sekta ya elimu.

Dkt. Kasululu alibainisha kuwa wadau wanalo jukumu la kuhakikisha mkoa wa Rukwa unapiga hatua kubwa kwenye ufaulu na kuboresha mazingira ya utoaji elimu.

Akitoa taarifa ya hali ya elimu mkoani Rukwa katika kipindi cha mwaka 2020/2021 Afisa Elimu Mkoa huo Samson Hango alisema asilimia za ufaulu wa wanafunzi katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi haujaongezeka lakini mwaka 2020 ulikuwa asilimia 80.3 na mwaka 2021 ulikuwa asilimia 80.2

Kwa upande wa mtihani wa Kidato cha Nne Hango alitaja ufaulu umeongezeka toka asilimia 87.7 mwaka 2020 hadi asilimia 89.7 mwaka 2021 ambapo aliwapongeza walimu, wanafunzi ,wazazi na wadau wote kwa mafanikio hayo.

Aidha, Afisa Elimu huyo aliongeza kusema Mkoa wa Rukwa una jumla ya shule za msingi 382 zikiwa na wanafunzi 336,951 na sekondari 97 zenye wanafunzi 52,746.

Kuhusu changamoto ya upungufu wa walimu Hango alisema mahitaji ya mkoa ni kwa shule za msingi ni walimu 7,322 waliopo ni 4,163 na kufanya upungufu wa walimu 3,159 sawa na asilimia 43.

Hango aliongeza kuwa ikama ya walimu wa masomo ya sayansi katika shule za sekondari mahitaji ni walimu 935 ambapo waliopo ni 465 na upungufu ni walimu 470 na kusema mkoa unaendelea na mikakati wa kutafuta walimu wengi.

Kikao hicho cha wadau wa elimu kimehudhuriwa na wajumbe zaidi ya 300 wakiwemo maafisa elimu , walimu, wawakilishi wa taasisi za kielimu na vyuo, wakuu wa Idara, wakurugenzi wa halmashauri ,wakuu wa wilaya, viongozi wa dini na kamati ya ulinzi mkoa.

Mwisho.

Comments