Mabaharia 11 wanusurika kifo baada ya meli kuzama katika ziwa Tanganyika.

 


MABAHARIA 11 wa meli ya MV.Mbayamwezi ya Burundi wameokolewa baada ya meli yao kuzama ziwa Tanganyika ikitokea Zambia kuelekea nchini Burundi.

Akitoa taarifa kwa Waandishi wa habari jana Kamanda wa polisi mkoani Rukwa  Willium Mwampagale alisema kuwa meli hiyo ya MV.Mbayamwezi yenye usajili wa namba  BY 0074 mali ya Rafiki Ibrahimu chini ya kampuni ya Red marine ya Burundi ilizama ziwa Tanganyika katika maeneo ya Kabwe wilayani Nkasi mkoani Rukwa  baada ya kupigwa na dhoruba kali februari 17 majira ya saa 5 asubuhi.


Alisema kuwa Meli hiyo ilitoka Mpulungu nchini Zambia  kuelekea Nchini Burundi tarehe 16 ya mwezi huu ikiwa ibebeba malighafi ya kutengenezea saruji ikiwa na Mabaaria 11 ambapo Wakongomani ni 6,Warundi 5 na Mtanzania 1 ndipo kesho yake walipofika eneo la Kabwe wilayani Nkasi walikumbana na dhoruba kali iliyopelekea meli hiyo kuyumba na kuzama.

Kamanda Mwampaghale alidai kuwa baada ya meli hiyo kuzama  mabaharia hao walivaa vifaa vya kujiokolea  na walikaa majini masaa 24 hadi walipokwenda kuokolewa na askari Polisi,JWTZ  ikiwa ni pamoja na Wavuvi.

Alisema jitihada za kuwaokoa Mabaharia hao zilizaa matunda ambapo walikimbizwa katika kituo cha afya Kirando kwa matibabu na walipata huduma ya kwanza na kupata nafuu na hadi sasa wanaendelea vizuri.

Capteni wa meli hiyo Ramadhan Katambo  Morris alidai kuwa baada ya meli hiyo kuzama yeye alikua ni mtu wa kwanza kutoka ndani ya meli hiyo na kupiga mbizi huku akipiga mayowe ya kuomba msaada ndipo wavuvi na wengineo walijitokeza kwenda kutoa msaada wa kumuokoa na kuwaokoa wengine.

Alisema kuwa meli hiyo yenye uwezo wa kubeba  tani 18 siku hiyo ilibeba mzigo wa tani 17 na kuwa uzito ulikua sahihi bali ni upepo tu uliwayumbisha na mwisho wa siku meli yao ikazama

Mganga mfawidhi wa kituo cha afya Kirando Benedict Tilamasi alikiri kuwapokea Mabaharia hao wakiwa 11 huku sita kati yao wakiwa mahututi na kuwa baada ya kuwapatia huduma ya kwanza na kuendelea na matibabu mengine afya zao zimeendelea kuimalika.

Alisema wote sasa wapo vizuri kiafya ambapo mmoja wao ndiyo bado afya yake haijaimarika na wanaendelea kumpatia matibabu zaidi.

 

Comments