HALMASHAURI TOENI FEDHA KUTEKELEZA AFUA ZA LISHE KWA WATOTO CHINI YA MIAKA 8

 

Baraka lusajo – Rukwa.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti amezionya halmashauri za mkoa huo kwa kutokutoa fedha za utekelezaji wa afua za lishe katika kipindi cha Octoba hadi Desemba 2021.

Ametoa onyo hilo jana (25.02.2022) wakati akiongoza kikao cha tathmini ya mkataba wa shughuli za lishe kipindi cha Julai hadi Desemba 2012 kilichofanyika mjini Sumbawanga ambapo halmashauri zote nne ziliripotiwa kutoa fedha za lishe asilimia 17.5 tu hatua inayokwamisha shughuli za lishe.


“Leo ndio siku ya mwisho nisisikie kuwa Afisa Lishe anasema hajapewa fedha za kutekeleza shughuli wakati mkoa bado una tatizo la udumavu na utapiamlo .Wakurugenzi nendeni mkabadilike .Suala la lishe ni agenda muhimu kwa uhai wa watu wetu pamoja na watoto wetu” alisisitiza Mkirikiti.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Katibu Tawala Mkoa ambaye pia ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Bonoface Kasululu ilionyesha kuwa halmashauri za Sumbawanga Manispaa, Sumbawanga Vijijini, Nkasi na Kalambo zimetoa asilimia 17 na kupelekea mkoa uwe kwenye rangi nyekundu.

Dkt. Kasululu aliongeza kusema matokeo ya ujumla yanaonesha kuwa mkoa wa Rukwa una wastani wa alama asilimia 87 ambapo kiasi hicho kimechangiwa na kutokutolewa kwa fedha za afua za lishe kwa upande wa halmashauri.

“Asilimia ya bajeti ya halmashauri iliyotumika kutekeleza shughuli za lishe kati ya iliyotengwa rangi nyekundu ni asilimia 17.5 kiashiria hiki kinaendelea kufanya vibaya zaidi ikilinganishwa na matokeo ya asilimia 54 kipidi cha mwaka 2020/2021” alieleza Dkt. Kasululu.

Taarifa ya tathmini kwa kiashiria cha asilimia ya fedha zilizotumika kwa shughuli za lishe katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2021 kwenye halmashauri na asilimia zake kwenye mabano Manispaa ya Sumbawanga (0.0), Sumbawanga DC (18.9), Nkasi DC (0.0) na Kalambo DC (47.7) hatua inayofanya mkoa kuwa na jumla ya asilimia 17.5

Mmoja wa Maafisa Lishe toka Halmashauri ambaye hakutaka jina litajwe alisema “tumekuwa tukiandika madokezo kuomba fedha za shughuli za lishe lakini hatupatiwi bila kupewa sababu. Octoba –Desemba  2021 niliomba shilingi 800,000 lakini hadi leo sijajibiwa na kazi zimesimama” alisema mtaalam huyo.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Jukwaa la Lishe Tanzania (PANITA) Aron Isaack alisema licha ya mkoa wa Rukwa kushika nafasi ya 13 kati 26 mwaka 2020/21 bado kuna changamoto kubwa ya shughuli za lishe kutopewa kipaumbele hatua inayosababisha utapiamlo na udumavu kuendelea.

Isaack aliongeza kuwa kunahitajika utashi wa kisiasa ili kutekelezwa kwa mkataba wa lishe miongoni mwa viongozi na watendaji wa serikali wakiwemo Waganga Wakuu wa Wilaya za Rukwa.

“Tunaishukuru serikali kwa kusimamia suala la lishe hasa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 iliyotamka suala la lishe kupewa kipaumbele “alisema Isaack.

Alisema lengo la serikali ni kuhakikisha watoto hususani wenye umri chini ya miaka 5 wakuwa na lishe bora  na kufikia maelengo y kutokomeza uduma  kwa watoto ambao ni taifa la kesho.

Kwa mujibu wa taarifa ya lishe iliyotolewa na Wizara ya Kilimo Desemba 2020 ilionesha kuwa mikoa inayoongoza kwa uzalishaji mazao ya chakula ndio ina kiwango kikubwa cha udumavu unaotokana na utapiamlo ikiwemo Rukwa (47.9), Njombe (53.6) na Iringa (47.1) huku watoto wenye umri chini ya miaka 8 wakitajwa kuathirika zaidi na tatizo la udumavu.

Mwisho.

Comments