Na Baraka Lusajo - Rukwa.
Wakandarasi
wanaotekeleza miradi ya maji mkoani Rukwa wametakiwa kuwa waadilifu na
wazalendo ili wananchi wapate maji vijijini na mijini kwa ustawi wa jamii hatua
itakayo ondoa kero za ukosefu wa maji.
Kauli hiyo
imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti wakati aliposhuhudia
hafla ya utiaji saini mikataba minne ya miradi ya maji kwa kati ya Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini
(RUWASA) na wakandarasi mjini Sumbawanga.
“Miradi hii
haihitaji stori, tunahitaji siku 180 za mkataba zitumike kukamilisha ujenzi wa
miradi ya maji huku tukizingatia matumizi sahihi ya fedha pamoja na uadilifu “alisema
Mkirikiti.
Katika hafla hiyo
mikataba minne ya ujenzi wa miradi ya maji yenye thamani ya shilingi
1,383,238,518 itakayotekelezwa kwa siku 180 katika wilaya za Nkasi na
Sumbawanga.
Akitoa taarifa
kabla ya utiaji saini, Meneja wa Mkoa wa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira
Vijijini (RUWASA) Mhandisi Boaz Matundali alisema jumla ya miradi 19 imetangazwa
katika mwaka huu wa fedha ambapo minne kati yake imepata wakandarasi.
Mhandisi Boaz
alitaja miradi itakayosainiwa kuwa ni ujenzi wa mradi wa maji Msanda Muungano
wilaya ya Sumbawanga wenye thamani ya shilingi Milioni 295.7 chini ya
mkandarasi Kiluswa Building Contrators ya Sumbawanga.
Miradi mengine
itatekelezwa katika wilaya ya Nkasi ambayo ni ujenzi wa mradi wa maji
Lyazumbi (shilingi Milioni 308.4),
ujenzi wa mradi wa maji Kacheche (shilingi Milioni 385.0) na mradi wa maji
Masolo (shilingi Milioni 395.9) yote itatekelezwa na mkandarasi Consel
Construction and Engineering Services ya Mwanza.
Katika hatua
nyingine Mhandisi Boaz alisema katika mwaka huu RUWASA mkoa wa Rukwa unatumia
wakandarasi katika kutekeleza miradi yake tofauti na ilivyokuwa mwaka uliopita
ambapo miradi ilitumia force account na nguvu za wananchi hivyo wanategemea
itakamilika ndani ya kipindi cha siku 180 za mkataba.
Comments
Post a Comment