MADARASA 332 KUKAMILIKA IFIKAPO DESEMBA –RC MKIRIKITI


Halmashauri za mkoa wa Rukwa zimetakiwa kuhakikisha miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa kwenye shule za sekondari na msingi chini ya Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 yanakamilika ifikapo Desemba mwaka huu.

“Maelekezo yangu ni kuwa tupo nyuma ya ratiba ya utekelezaji miradi hii hivyo nataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote kuongeza kasi ya usimamizi na ufuatiliaji ili fedha zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan zipate matokeo tarajiwa kabla ya Desemba 15 madarasa yote yawe yamekamilika kujengwa” alisema Mkirikiti.

Akiwa kwenye ziara ya kukagua miradi ya elimu na afya kwenye Halmasahauri ya wilaya ya Kalambo na Sumbawanga , Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti aliagiza Wakurugenzi kuhakikisha miradi hiyo inakamilika pasipo visingizio kwa kuwa fedha tayari zipo kwenye akaunti zao tangu mwezi Octoba mwaka huu.


Mkirikiti aliongeza kusema, katika kutekeleza miradi hiyo ya ujenzi ni budi halmashauri zikazingatia matumizi sahihi ya fedha kwa kuwa na miradi bora na endelevu ambapo msisitizo vifaa kama saruji, mbao na mabati vinunuliwe kwa kuzingatia bei ya soko.

Aliongeza kusisitiza ushirikishwaji wa kamati za ujenzi kwa kila mradi kulingana na Mwongozo ulitolewa na Ofisi ya Rais Tamisemi ambapo wananchi wanatakiwa kutambua na kushiriki kwenye miradi hii.

Kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 Mkoa wa Rukwa ulipokea jumla ya shilingi 8,940,000,000 ambapo kati hizo shilingi 6,800,000,000 zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 332 ya shule za sekondari na madarasa 74 kwenye vituo shikizi pamoja na mabweni ya walemavu.

“Jumla ya madarasa 259 kwa shule za sekondari yenye thamani ya shilingi 5,180,000,000, vyumba vya madarasa katika vituo shikizi vya shule za msingi 73 yenye thamani ya shilingi 1,460,000,000 na mabweni mawili kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu yenye thamani ya shilingi 160,000,000 yatajengwa kupitia mradi huu kwenye mkoa wa Rukwa” alisisitiza Mkuu wa Mkoa Mkirikiti.

 Aidha,  kiasi cha shilingi 2,140,000,000 kati Bilioni 8.940  zitatumika kwa ajili ya sekta ya afya kwa ajili ya ujenzi wa majengo (2) majengo ya huduma za dharura (EMD) kwa Milioni 600 na ujenzi jengo moja la huduma za wagonjwa mahututi (ICU) kwa shilingi Milioni 100 wilaya ya Kalambo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mkoa pia utatekeleza ununuzi mashine za Mionzi tatu (3) (X-Ray) kwa shilingi Bilioni 1.26 na ujenzi wa nyumba mbili (2) za watumishi wa afya  Nkasi na Kalambo kwa shilingi Milioni 180.

Comments