Asilimia 43 ya watoto wenye umri chini ya miaka 5 watajwa kutofikia hatua ya ukuaji kutokana na utapiamlo.



Na Baraka Lusajo- Dodoma.

Waziri wa afya maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto Doroth Gwajima amesema asilimia 43 ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano wako kwenye hatari ya kutofikia hatua timilifu ya ukuaji kutokana na uwepo wa viashiria mbalimbali ikiwemo utapia mlo, pamoja na miundombinu duni ya kifamilia huku watoto 270 waliochini ya umri huo  hupoteza maisha kila mwaka  kutokana na lishe duni.

Ameyabainisha hayo jana kupitia uzinduzi wa program jumuishi ya taifa ya malezi ,makuzi na maendeleo ya awali ya watoto wenye umri chini ya miaka 5 na kubainisha kuwa Malezi ya watoto chini ya miaka nane yanakabiliwa na changamoto mbalimbali, hivyo kusababisha watoto wengi kushindwa kukua na kufikia utimilifu wao.

‘’ Tanzania ni moja ya nchi zenye uchumi wa kati wa chini ambapo asilimia 43 ya watoto wapo kwenye hatari ya kutofikia hatua timilifu ya ukuaji na maendeleo yao kutokana na viashiria mbalimbali vikiwemo utapiamlo, kukosekana kwa uhakika wa chakula, msongo wa mawazo katika familia, miundombinu duni katika familia, uhaba wa rasilimali pamoja na utekelekezaji na unyanyasaji wa watoto’’alisema Gwajima.


Tanzania ni moja kati ya nchi za Afrika yenye idadi kubwa ya watoto wenye utapiamlo.  Kwa mujibu wa Utafiti wa hali ya lishe uliofanywa na Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC) kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya Mwaka 2018, ilibainika kuwa, zaidi ya watoto 2,600,000 chini ya miaka mitano Tanzania wamedumaa; idadi kubwa wakiwa katika Mikoa 11 ambayo ni; Dar-es-Salaam, Kagera, Kigoma, Mara, Dodoma, Geita, Tanga, Ruvuma, Mbeya, Morogoro, na Tabora.

 

 

Comments