Na mwandishi
wetu- Kigoma
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mheshimiwa Thobias Andengenye amesema kuwa adhabu kali zitatolewa kwa wasafirishaji wanaokiuka Sheria ya Udhibiti Uzito wa Magari pamoja na makosa tofauti yanayohusisha huduma za mizani.
Ameyasema hayo wakati akifungua semina ya mafunzo kwa wadau wa usafirishaji kuhusu Sheria ya Udhibiti Uzito wa Magari ya Afrika Mashariki ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018 inayofanyika kwa siku moja mkoani humo.
“Anaezidisha
uzito anaweza pia akasababisha ajali, hii inaweza ikapelekea akafungiwa shughuli
za usafirishaji kwa muda au hata kufungiwa moja kwa moja. Adhabu tofauti na
uzidishaji uzito wa magari ni faini ya Dola za Kimarekani 15,000 au kifungo cha
miaka mitatu. Adhabu hiyo pia itahusisha watumishi wa mizani wanaokula njama na
wasafirishaji ambao sio waaminifu.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mjini, Esther Mahawe, ameipongeza Serikali, kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Ujenzi), kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara nchini na kuwataka wadau wa usafirishaji kushiriki kikamilifu katika jitihada za Serikali za kuleta maendeleo nchini.
Awali, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Kigoma, Mhandisi Narcis Choma alimuambia Mkuu wa Mkoa wa Kigoma kuwa mafunzo hayo yanalenga kuongeza uelewa wa sheria ya Udhibiti Uzito wa Magari kwa wadau wa usafirishaji ili nao waweze kushiriki kikamilifu katika ulinzi wa miundombinu ya barabara nchini, na kuhakikisha kuwa zinadumu kwa muda uliokusudiwa.
Kwa upande wake msimamizi wa Mizani kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Leonard Saukwa amewaambia waandishi wa habari kuwa, adhabu zitokanazo na uzidishaji uzito wa magari zinatofautiana kulingana na uzito unaozidishwa kwenye gari husika.
“Hata hivyo, yapo makosa ambayo wadau wa usafirishaji wanayatenda mara kwa mara tofauti na uzidishaji uzito katika magari, na wanapokiri makosa hayo basi wasafirishaji hao hutozwa faini ya dola za Kimarekani 2,000” amesema Mhandisi Saukwa.
Nao wadau wa usafirishaji wanaohudhuria mafunzo hayo mkoani Kigoma, wamesema kuwa mafunzo hayo yatakuwa chachu kwa wao kudhibiti uzito wa magari yao kwa kubeba mzigo isiyozidi uzito, na hivyo kuepusha uharibifu wa mara kwa mara wa magari yao lakini pia kuepusha uharibifu wa barabara ambazo Serikali inatumia fedha nyingi kuzijenga pamoja na kuzikarabati.
Semina ya
mafunzo kuhusu Sheria ya Udhibiti Uzito wa Magari ya Afrika Mashariki ya mwaka
2016 na kanuni zake za mwaka 2018 inahusisha wamiliki wa vyombo vya
usafirishaji, madereva, pamoja na wadau wengine wa usafirishaji kutoka
Serikalini pamoja na sekta binafsi.
Comments
Post a Comment