Jeshi la Magereza mkoani Rukwa kuzindua mabweni 3 ya kulala wafungwa na mahabusu

Jeshi la Magereza Mkoa wa Rukwa katika kuadhimisha Miaka 60 ya Uhuru limefanikiwa kuzindua mabweni matatu mapya ya kulala wafungwa na mahabusu kwenye Gereza la Mahabusu Sumbawanga yakiwa na uwezo wa kulala watu Mia mbili (200).

Akizindua mabweni hayo jana (23.11.2021) Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti amelipongeza Jeshi hilo kwa kuboresha mazingira ya kuhifadhi wafungwa na mahabusu  hatua itakayopunguza msongamano.

"Gereza hili la mahabusu Sumbawanga lilianzishwa mwaka 1927 na wakoloni na hadi leo lilikuwa halijafanyiwa maboresho .Leo tukiwa kwenye shamrashara za  maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru wa Taifa tunazindua mabweni haya hivyo ni furaha kuonesha tumepiga hatua kubwa za kimaendeleo" alisema Mkirikiti


Katika hatua nyingine Mkirikiti alitoa wito kwa vyombo vya utoaji haki ikiwemo mahakama na Jeshi la Polisi kuharakisha michakato ya upelelezi na usikilizwaji mashauri mahakamani ili watuhumiwa waweze kupata haki zao mapema hatua inayosaidia kupunguza msongamano magerezani.

"Vyombo vya kutoa haki vifanye kazi zake haraka na kwa uaminifu ili haki itendeke na wasio na hatia basi wasiendelee kukaa mahabusu bali waruhusiwe kurejea uraiani kuendelea na ujenzi wa Taifa" alisisitiza Mkuu huyo wa Mkoa wa Rukwa.

 

Kwa upande wake Mkuu wa Gereza la  mahabusu Sumbawanga Mrakibu wa Magereza ( SP) Melkior M. Komba alisema kukamilika kwa maselo (mabweni) hayo matatu kunaongeza uwezo wa kuhudumia mahabusu na wafungwa ambao kwa sasa wapo 422 huku uwezo uliokuwepo ni kuhudumia watu 200 pekee.

SP Komba alisema mabweni hayo maselo hayo matatu yatakuwa na uwezo wa kulaza mahabusu 200 kwa wakati mmoja hatua itakayosaidia kuondoa msongamano gerezani hapo.

Aliongeza kusema mradi huo wa maselo umegharimu shilingi Milioni 187 kati ya hizo shilingi Milioni 62 zilitolewa na Kamishna Jenerali wa Magereza (CGP) Meja Jenerali Suleiman Mzee huku wadau wakichangia shilingi Milioni 124.

Aidha,SP Komba alisema kazi ya ujenzi wa mradi huo imefanikishwa na uwepo wa timu nzuri ya  wataalam wa ujenzi ambao ni Askari na wafungwa hatua iliyosaidia kupunguza gharama za mradi huo ambazo awali zilikadiliwa kufikia shilingiilioni 256.

Kwa upande wake Mkuu wa Magereza Mkoa wa Rukwa Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Motrais Mwakilima akielezea mafanikio hayo ya Miaka 60 ya Uhuru alisema ni kutokana na jitihada za viongozi Wakuu wa Jeshi  Waliopo sasa na wale ambao walipata nafasi huko nyuma kulitumikia Jeshi .

ACP Mwakilima aliongeza kusema kuwa Jeshi la Magereza linawashukuru wadau na wananchi wote kwa kuendelea kuliunga mkono hata kufanikisha Miradi yake ikiwemo ujenzi wa masero haya katika Gereza Sumbawanga.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Sumbawanga,Mkuu wa Wilaya hiyo Sebastian Waryuba alipongeza jitihada za kuboresha mahala pa kupumzika  wafungwa na mahabusu lakini akatoa wito kwa wannachi kuepuka kujihusisha na vitendo vya kiuhalifu vitakavyopelekea wajikute wenye mikono ya vyombo vya dola.

"Kwa kuboresha mahala pa kulala wafungwa isiwe ni kigezo cha watu kukimbilia hapa bali tuendelee kuelimisha wananchi kuepuka vitendo vya kihalifu na uvunjifu wa amani ili wasifanye makosa yatakayopelekea kuwekwa mahabusu au kifungoni" alisema Waryuba.

Comments