RC MKIRIKITI: NATAKA FEDHA ZA MIRADI ZISICHEZEWE OVYO





Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti ameonya watendaji wa serikali wilayani Kalambo kutotumia vibaya fedha za miradi ya maendeleo zinazotolewa na serikali.

Akiwa kwenye ziara ya ukaguzi wa miradi wilayani Kalambo Mkirikiti hakuridhishwa na namna fedha shilingi milioni 60 zilivyotumika katika ujenzi wa madarasa matatu Matai sekondari

"Nataka kuona fedha za umma zinazotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan zinatumika kwenye miradi mipya iliyopangwa wala si kwa miradi viporo kwenye halmashauri yenu ya Kalambo. Sijafurahi kuona mradi huu wa majengo matatu ya darasa shule ya sekondari ya wasichana Matai kutokamilika licha fedha zote milioni 60 kuisha" alisema Mkirikiti 


Mkirikiti  alibainisha kuwa hataki kuona fedha zilizotolewa na serikali kwa ajili ya utekelezaji  mpango wa maendeleo na mapambano dhidi ya UVIKO-19 zitumike kwenye miradi ya zamani bali halmashauri  ikamilishe miradi viporo kwa kutumia fedha za mapato ya ndani.

"Kuweka tiles (marumaru) kwenye darasa siyo mbadala wa kutoweka madawati na meza. Tafuteni fedha shule hii ikamilike" aliagiza Mkirikiti.

Kufuatia hali hiyo Mkuu huyo wa Mkoa aliagiza viongozi wa wilaya hiyo kuongeza umakini kwenye usimamizi wa miradi pamoja na kuzingatia vigezo (BOQ) ili miradi iwe bora na kuendana na thamani ya fedha.


Akizungumza  jana kwenye eneo la mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo Shafii Mpenda alisema shule hiyo ya wasichana Matai inatarajiwa kuanza mwezi Januari 2022 kutokana na kutokamilika kwa vigezo vilivyotolewa na Mkaguzi Mkuu wa Elimu Kanda.

Mpenda amemthibitishia Mkuu wa Mkoa kuwa amejipnga kushirikiana na watendaji  wenzake kusimamia matumizi ya fedha kwenye miradi na kuepusha ubadhirufu unaoweza kusababisha miradi kutokamilika kwa wakati.

 

 

 

 

 

Comments