Mwenge Wa Uhuru Wazindua Miradi 6 Wilayani Kalambo

 Na Baraka Lusajo- Kalambo

Kiongozi wa Mbio maalum za Mwenge wa Uhuru 2021 Luteni Josephine Mwambashi ameagiza kukamilishwa haraka kwa zahanati ya kijiji cha Mbuza wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa ambayo iliibuliwa na kujengwa na wananchi ili wapate uhakika wa huduma za afya.

Kiongozi huyo wa Mwenge wa Uhuru amepongeza jitihada za wananchi hao walioamua kujichangisha nguvu zao hatua iliyowezesha waanze ujenzi wa zahanati hiyo mwezi April mwaka huu na tayari wametumia Shilingi 49,566,760 katika kujenga zahanati ambayo imefikia hatua ya umaliziaji baada ya lipu na bati kukamilika.



 Luteni Mwambashi alisema hayo (21.09.2021) wilayani Kalambo wakati mwenge wa uhuru uliotembelea kukagua mradi wa Zahanati ya Kijiji Cha Mbuza.

“Mwenge wa Uhuru upo tayari kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa zahanati hii ya kijiji cha Mbuza baada ya kuridhishwa na kazi iliyofanywa na wananchi kwa kuchangia fedha pia nguvu kazi ili wapate maendeleo”. alisema Luteni Mwambashi.


Aliongeza kuwa kitendo hicho cha kujenga zahanati ni uzalendo mkubwa uliooonyeshwa na wananchi kuunga mkono jitihada za serikali kufikisha huduma karibu na kumuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kalambo kuhakikisha zahanati hiyo inakamilika kabla ya mwaka 2021 kuisha.

Taarifa ya Halmashauri ilionyesha kuwa kati ya fedha hizo zilizotumika kujenga  wananchi wamechangia Shilingi 23,326,000,   halmashauri ya Kalambo ikichangia shilingi 24,656,260 na washirika wa maendeleo wamechangia Shilingi 1,584, 5000.

Katika hatua nyingine Kiongozi huyo wa Mbio za maalum za Mwenge wa Uhuru aliwasihi wananchi wa kijiji Msanzi kuhakikisha wanajitokeza kwenye vituo vya afya kupata chanjo dhidi ya UVIKO 19 ili kujikinga na ugonjwa wa Korona.


Alitoa rai hiyo mara baada ya mwenge kufika Katika kijiji Cha Msanzi kwa ajili ya kutembelea miradi ya maendeleo.

Ukiwa kijijini Msanzi , Mwenge wa Uhuru umeweka jiwe la msingi la msingi la ujenzi wa vyumba viwili vya maabara katika shule ya sekondari Msanzi ambapo ujenzi wake umetumia shilingi 88,886,714 kati ya hizo serikali kuu imetoa shilingi 60,000,000 ,halmashauri shilingi 18,971,214 na wananchi wamechangia shilingi 9,915,500.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Tano Mwera amesema atahakikisha miradi ya maendeleo inasimamiwa kwa karibu ili thamani ya fedha na ubora wake uwanufaishe wananchi.

“Sisi wananchi wa wilaya ya Kalambo tunatambua kabisa kwamba Mbio za Mwenge wa Uhuru huhimiza maendeleo, amani na umoja miongoni mwa watanzania” alihitimisha Tano.


Comments