Dc Lijualikali awafuta kazi askari migambo watatu kwa kosa la kuunda magenge ya uharifu

Na mwandishi wetu - Nkasi

Mkuu wa wilaya Nkasi mkoani Rukwa Peter Lijualikali amewafuta Kazi askari Mgambo watatu wa kijiji cha Swahila kata ya Mkwamba ikiwa ni pamoja na kumvua madaraka kaimu afisa mtendaji wa kijiji hicho kwa kosa la kuunda genge la uhalifu kupitia ofisi ya serikali ya kijiji kwa kuwabambikiza kesi Wananchi na kuwatoza faini kinyume cha sheria ikiwa ni pamoja na kutoa adhabu ya viboko kwa watuhumiwa wa Makosa mbalimbali.


 Uamuzi huo umetolewa jana kwenye mkutano wa hadhara baada ya mkuu huyo wa wilaya kupokea kero kutoka kwa Wananchi wa kijiji hicho ambapo wamesema kuwa kijiji hicho wameunda baraza la kijiji la kimila ambalo limejitungia sheria kinyume cha sheria na iliyopelekea kunyanyasika wananchi kwa kupewa tuhuma na kuwekwa mahabusu na kupigwa faini Kuanzia Tshs, 300,000 hadi milioni 1 ili kuachiwa.

Mmoja wa Wananchi hao Jellad Boniface alisema mbele ya mkuu wa wilaya kuwa yeye alipata adhabu ya kupigwa fimbo na kaimu afisa mtendaji wa kijiji hicho Yohana Simbeye na kupigwa faini ya Tshs, 400,000 kwa kosa la kuzozana na mkewe nyumbani kwao na kuwa wameshitakiwa na Jamhuri kwa kosa hilo na alilipa faini hiyo bila hata ya kupewa Risiti.

Redemita Anset alisema kuwa mmewe alikamatwa kwa kosa la kulima bangi na alipotaka kuthibitishiwa kosa hilo alionyeshwa picha ya shamba hilo kwenye Simu hivyo hakutakiwa kujitetea ndipo alipopewa adhabu ya kupigwa fimbo na askari Mgambo na kulazimika kulipa faini ya Tshs, 600, 000.

 Wananchi waliweza kutoa malalamiko mengi na kubwa la kuchapwa viboko wakiwemo Wanawake ambao walikua wakikutwa na Makosa mbalimbali na kwa wale wasiokuwa na fedha ya kulipa faini na Wana mifugo nyumbani kwao ofisi ya kijiji utafuta wateja wa mifugo yao na kuiuza ili watuhumiwa waweze kuachiwa kutoka katika mahabusu ya kijiji.

Kufuatia hari hiyo mkuu wa wilaya Peter Lijualikali aliamua kuwafukuza Kazi askari Mgambo watatu wa kijiji hicho ambao ni Robert Tito, Kulwa Madeni na Serina Kambaulaya na kumvua madaraka ya kukaimu Uafisa mtendaji wa kijiji Yohana Simbeye huku mwenyekiti wa kijiji hicho Gefrin George akikabidhiwa kwa mwenyekiti wa CCM wa wilaya Salum Sudi kwa kumchukulia hatua za kididhamu ikiwa ni pamoja na kumvua uanachama kwa kosa la kuunda genge la uhalifu katika ofisi yake na kutengeneza sheria ndogo ambazo hazijapitishwa na halmashauri na kuwakandamiza Wananchi.

> Kaimu mkurugenzi mtendaji wa wilaya Asubisye Rajae alisema kuwa kutokana na malalamiko hayo aliyoyasikia toka kwa Wananchi atawachukulia hatua za kinidhamu Watumishi wake waliohusika katika vitendo hivyo viovu ambao ni kaimu afisa mtendaji wa kijiji hicho ambaye pia ni afisa kilimo wa kata na afisa mtendaji wa kata hiyo kwa kosa la kushindwa kuwajibika na kuruhusu vitendo haramu kufanyika kwenye ofisi ya serikali.

 Naye mwenyekiti wa CCM wilaya Salum Sudi alidai kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimefedheheshwa Sana kwa kitendo cha mwenyekiti wa kijiji anayetokana na CCM kujiingiza kwenye vitendo vya kuwakandamiza Wananchi na kufanya uonevu hadharani na kuwa Chama kitachukua hatua za haraka dhidi yake.

 Uongozi wa kijiji cha Swahila umekuwa ukilalamikiwa na Wananchi kwa kipindi kirefu ndipo mkuu huyo wa wilaya Alipoamua kwenda katika Kijiji hicho ili kuweza kupata ukweli wa malalamiko hayo na kuweza kubaini uovu mkubwa unaofanya na ofisi ya serikali ya kuwanyanyasa Wananchi

Comments