Ziara Ya Rais Samia Suluhu, Kenya Na Tanzania Zanufaika.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan Jumatano alikamilisha ziara ya kikazi ya siku mbili nchini Kenya huku pakiwa na matumaini kati ya nchi hizi mbili kwamba ziara hiyo itafungua sura mpya katika undugu na ujirani.

Ziara ya Samia imeonekana kuwa imechangia sehemu kubwa kufungua milango ya kibiashara kati ya nchi hizo mbili na kuondoa dhana na hofu zilizokuwepo kwamba uhusiano kati ya nchi hizo mbili ulikuwa ukizidi kudorora . Kupitia kauli zake katika kila fursa aliyopata kuzungumza ,Rais Samia alisisitiza umuhimu wa mataifa hayo mawili kushirikiana bila kuwepo ushindani ,kauli au vitendo vya kukwazana .

Wakati akilihutubia Bunge la Kenya mara baada ya kumalizika kwa kongamano la wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya Rais Samia alisema;

"Binafsi huwa nashangazwa sana na wale wanaodhani Kenya na Tanzania ni wapinzani, mbaya zaidi ni kule kuamini kwao kwamba hilo linawezekana tu mmoja wetu kumwangusha mwenzake, hawa ni watu wenye mioyo ya choyo, maono mafupi na akili mbovu."

Ni bahati mbaya kuwa watu hawa wapo katika pande zote mbili, Kenya na Tanzania hutokea pia wachache wao wakawa ni watumishi wa Serikali zetu na hata wanasiasa wa pande mbili za nchi zetu. Bahati nzuri ni kuwa si wengi ndio maana uhusiano ya nchi zetu mbili unatimiza miaka 56 sasa," amesema Samia.

Comments