Mkuu Wa Majeshi Tanzania Aahidi Utii Kwa Rais Samia Suluhu Hassan

 

Mkuu wa Majeshi ya Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo ameahidi utiifu kwa Rais Samia Suluhu Hassan na Amirijeshi Mkuu.

Bw. Mabeyo amemhakikishia kuwa ulinzi wa nchi na mipaka yake ni salama na vitaendelea kumlinda, kumtii kama Amirijeshi mkuu na kutekelezamajukumu yake kwa mujibu wa katiba ya Tanzania.

‘’Tunakuahidi utiifu, uadilifu na uaminifu mkubwa kama ilivyo ada ya mila na desturi ya majeshi yetu katika awamu zote zilizopita kwa manufaa ya ulinzi, usalama na ujenzi wa taifa letu’’. Alisema Jenerali Mabeyo.

Jenerali Mabeyo alisema hayo mjini Chato wakati akimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuapishwa kuwa Amirijeshi Mkuu.

Kuhusu namna alivyomfahamu na kufanya naye kazi hayati Magufuli Jenerali Mabeyo alisema;

‘’Aliviamini na kuvipenda vyombo vya ulinzi na usalama alihakikisha kuwa anaviwezesha kwa mahitaji ya kiutendaji na utawala ili viweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na weledi mkubwa.’’

‘’Alisema hatuwezi kuwa na vyombo vya ulinzi imara bila kuwa na uchumi madhubuti, hatuwezi kutegemea misaada ya kuimarisha vyombo vyetu lazima tuimarishe uchumi wetu ili tuweze kuimarisha vyombo vyetu vya ulinzi na usalama.’’

Mabeyo amesema walishiriki katika kulinda mgodi wa Tanzanite, na  kulinda, kujenga ukuta kuzunguka mgodi huo.

 Hata hivyo kwa upande wake Rais wa awamu ya nne wa Tanzania Jakaya Kikwete amesema taarifa ya kifo ilikuwa jambo gumu kulipokea na kulikubali.

Akieleza mahusiano yake na hayati Magufuli tangu alipokuwa waziri wake, Kikwete amesema alikuwa jembe lake.

Nilipokuwa Rais, Magufuli alikuwa Waziri wangu kwa miaka 10, alikuwa mmoja wa mawaziri niliowaamini na kumtumaini.

‘’Alikuwa jembe langu ndio maana nilimuweka kwenye wizara tatu zilizokuwa ngumu ili anyooshe mambo.’’ Alisema Kikwete.

‘’Yalikuwa matumaini yangu na matarajio yangu angemaliza kipindi chake cha uongozi salama, akastaafu na kuishi maisha marefu baada ya hapo na kupata nafasi ya kutuzika sisi watangulizi wake ambao ni kaka zake, hili la kututoka kabla ya kumaliza muhula wake na sisi kumzika yeye ni jambo ambalo sikuwahi kulifikiria kabisa.’’ Alisema Kikwete.

Amesema uongozi wake bado ulikuwa ukihitajika Tanzania, na kuwa alikuwa akitamani akamilishe kazi yake nzuri aliyokwisha ianza.

 

 

Comments