Je? Dkt Philipo mpango ni nani.



Dkt. Philip Mpango ambaye anatarajiwa kuapishwa leo kuwa makamu wa rais wa Tanzania alikua Waziri wa Fedha na Mipango katika Serikali ya Awamu ya Tano, ameteuliwa katika baraza la mwanzo la mawaziri la Rais John Magufuli.

Mwaka 2015 alikua mbunge wa kuteuliwa.

Bwana Mpango ni mzaliwa wa Kigoma, baba yake ni marehemu Isidori Nzabhayanga Mpango, ambaye alizaliwa Kijiji cha Kasumo, Wilaya ya Kasulu.

Dkt. Mpango alizaliwa hapo hapo Kasumo na ni kaka mdogo wa Askofu mstaafu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Tanganyika Magharibi - Kasulu mkoani Kigoma, Dk Gerard Mpango.

Kuanzia miaka ya 1990 hadi 2000, alifanya kazi akiwa mhadhiri mwandamizi wa uchumi katika kitivo cha Biashara (sasa Shule ya Biashara) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Alikuwa akifundisha "Microeconomics", "Macroeconomics" (kwa mwaka wa pili) na "Public Finance" kwa mwaka wa tatu na kozi za uzamili. (Kwa tafsiri yangu, Uchumi mdogo, Uchumi mkubwa na masuala ya Fedha za umma.).

Amewahi kuwa Mchumi Mwandamizi wa Benki ya Dunia, Mkuu wa Kamati ya kumshauri Rais Jakaya Kikwete wakati huo kuhusu masuala ya uchumi, Katibu binafsi wa Rais anayeshughulikia masuala ya uchumi, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, kabla ya kuhamishiwa Tume ya Mipango, Ofisi ya Rais.

Nyadhifa hizi zote amezishika wakati wa utawala wa Kikwete.

Hayati Magufuli alipoingia madarakani alimteua kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na baada ya siku chache akateuliwa kuwa Waziri wa Fedha na Mipango.

Katika uchaguzi wa mwaka 2020 alishinda kiti Cha ubunge jimbo la Buhingwe.

Dkt. Philip Isidory Mpango aliyetangazwa kuwa Makamu wa Rais mteule wa Tanzania ni mchumi wa kiwango cha juu .

 

Dk. Mpango hana tabia za kawaida unazoweza kuzihusisha na wanasiasa wa Afrika. Mpango ni msema kweli, mwadilifu, mcha Mungu na mtu ambaye anaamini katika vitendo kuliko maneno.

Sababu hizo, pamoja na uwezo wake kama mchumi, ndizo zilizomfanya abaki kuwa Waziri wa Fedha katika muda wote wa miaka sita ya utawala wa Rais Magufuli. Jambo hilo si dogo kwa sababu wizara hiyo ilikuwa ikiangaliwa kwa jicho la karibu na Rais Magufuli ambaye alijulikana kwa kutovumilia wateule wake ambao walionekana kutokidhi matarajio yake.

Dk. Mpango ni mwanasiasa wa bahati mbaya kwa sababu katika utumishi wake wa takribani miaka 40 serikalini, mara zote alitumika kama mtaalamu na aliingia kwenye siasa kwa kuteuliwa na Rais Magufuli kuwa mbunge na baadaye waziri miaka sita iliyopita.

Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 ulikuwa ni mara yake ya kwanza kuwania ubunge - bila shaka kwa kutosubiri tena kupata huruma ya Rais Magufuli ya kuteuliwa.

Umakamu Rais wa Mpango pia unaweka sawa baadhi ya kanuni ambazo haziandikwi lakini zimezoeleka katika desturi na utamaduni wa kisiasa wa Tanzania.

Yeye anatoka katika Mkoa wa Kigoma - mojawapo ya mikoa ya pembezoni ya Tanzania ambayo haijawahi kutoa Rais, Makamu wa Rais wala Waziri Mkuu. Uteuzi huu umetoa fursa kwa eneo ambalo halijawahi kutoa mmoja wa viongozi wakuu watatu wa Tanzania, kupata fursa hiyo.

 

 

Comments