WANAFUNZI 6 WAFARIKI KWA MATUKIO TOFAUT WILAYANI NKAS

 Na Israel  Mwaisaka,Nkasi


WANAFUNZI 6 wa shule mbalimbali za msingi wilayani Nkasi mkoani Rukwa wamefariki jana jioni  ambapo Wanne walipigwa na radi na wawili kugongwa na gari katika maeneo tofauti,ambapo watatu kati ya waliopigwa na radi ni wa familia moja.

Akizungumza kwenye mazishi ya Watoto Watatu wa familia moja katika kijiji cha Nkana kata ya Nkandasi mkuu wa wilaya Nkasi Said Mtanda alisema kuwa wilaya Nkasi ina majonzi makubwa ambapo jana tu ni watoto 6 wamepoteza maisha ambapo Wanne walipigwa na radi na wawili kugongwa na gari katika maeneo tofauti.

Alisema kuwa vifo hivyo vimeleta simanzi kubwa wilayani Nkasi na kuwaomba Wananchi kuondoa fikra zozote mbaya juu ya vifo hivyo kwani yote ni mapenzi ya Mungu.

Awali  kaimu afisa elimu wa wilaya Agnes Martin alisema kuwa licha ya Watoto watatu  wa familia moja kuuawa kwa radi  katika kijiji hicho cha Nkana pia kuna mwanafunzi mwingine wa shule ya msingi Nchenje naye alipigwa na radi wakati Wanafunzi wengine Wawili waligongwa na gari.

Aliwataja Watoto hao wa familia moja waliofariki kuwa ni Rita Remi Chiwalala (6) Mwanafunzi ya awali katika shule ya msingi Nkana,Macrida Chrisipine Mtepa (7) darasa la 1 na Exavery Lucas Chipamba (13) wa darasa la 5 na mwingine ni Kwilasa Siri (9) wa darasa la tatu shule ya msingi Nchenje ambaye alipigwa na radi jioni akiwa nyumbani kwao.

Pia aliwataja Wanafunzi wengine waliofariki kwa kugongwa na gari ni Boniphace Regius Sapi (8) wa darasa la pili  shule ya msingi Kipundukala na Debora Chulula (12) darasa la tatu shule ya msingi Chala.

Akisimulia mkasa huo kaimu afisa elimu kata ya Sintali Patrick Fute alisema kuwa radi hiyo iliyowapiga Watoto wa familia moja ilitokea majira ya saa 11 jioni walipokuwa wakicheza mchezo wa kitoto na walikua 11 na baada ya radi hiyo kushuka Watoto  hao watatu walifariki papo hapo.

mwisho

Comments