KATIBU WA AFYA AFARIKI KWATUMBUKIA KWENYE KISIMA WILAYANI NKASI

 

Na Israel Mwaisaka,Nkasi

KATIBU wa afya wa halmashauri ya wilaya Nkasi Ibrahimu Kashatila (29) amefariki dunia baada ya kutumbukia kwenye kisima kilichopo mjini Namanyere.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kaimu kamanda wa Polisi mkoani  Rukwa Theopista Mallya ni kuwa taarifa za kupotea kwa marehemu zilitolewa na mkewe January 23,2021 na juhudi za kumtafuta ziliendelea na ndipo January  27 majira ya saa 11:30 jioni zilitolewa taarifa za mwili wa kijana huyo kupatikana kwenye kisima akiwa amekufa.

Amesema kuwa marehemu alitoka nyumbani kwake januari 23 ya mwaka huu akienda matembezini na kuwa toka siku hiyo hakuonekana nyumbani wala kazini kwake na taarifa zilitolewa Polisi na juhudi za kumtafuta ziliendelea hadi pale mwili wake ulipopatikana kwenye kisima kilicho karibu na bar moja mjini Namanyere inakosadikika kuwa  alikua wakinywa pombe na ulipatikana baada ya siku 4.

Kamanda Mallya alisema kuwa uchunguzi wa jeshi la Polisi unaendelea ili kuweza kubaini chanzo cha kifo hicho na kuwa wao kama Polisi kwa sasa wanasubiri taarifa ya kitabibu ambayo wataiunganisha na taarifa za kiuchunguzi.

Alisema kuwa sasa  ni mapema sana kwao kuzungumza mambo kwa kina lakini uchunguzi ukikamilika watatoa taarifa nzima  ya tukio hilo.

Ndugu wa marehemu   walikabidhiwa mwili kwa ajiri ya mazishi baada ya hatua za awali za uchunguzi kukamilika

Mwisho                                     

 

Comments