Dc Ataka Wanaokwamisha Shughuli Za Maendeleo Kukamatwa.



MKUU wa wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa Calorus Misungwi ametoa siku tatu kwa viongozi wa serikali za vijiji vitatu vya kata ya Kisumba kuhamasisha wananchi kujitokeza kwenye shughuli za maendeleo ya ujenzi wa bweni la wanafunzi wa shule ya sekondari Chisenga.

Ameyasema hayo baada ya kutembelea ujenzi wa miradi ya maendeleo katika kata hiyo na kubaini kusua sua kwa ujenzi huo kutokana na wananchi pamoja na viongozi wa serikali za vijiji hivyo kususia ujenzi huo kwa madai ya fedha zilizoletwa na serikali zilikuwa kwa ajili ya malipo ya vibarua na mafundi.

 Kufuatia hali hiyo akawaagiza wenyeviti wa vijiji hivyo pamoja na watendaji kufika ofisini kwake na kusisitiza watendaji kuhakikisha wanawaweka ndani watu wote wanaogoma kushiriki kwenye shughuli za maendeleo.

 Kaimu mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo Erick Kayombo, amesema fedha zote zinazotolewa kwenye miradi hiyo ni kwaajili ya ujenzi, na kazi zingine zinazobakia zinatakiwa  kufanywa na wananchi.

“Shughuli zote ndogo ndogo katika utekelezaji wa miradi hii zinatakiwa kufanywa na wananchi mfano ubebaji mchanga, kubeba mawe na kuchimba misingi zote hizo kwa ujumla wake zinafanywa na wananchi,

Aidha aliwataka wananchi kuendelea kushiriki kwenye shughuli za maendeleo kwa lengo la kuwezesha miradi hiyo kukamilika kwa haraka.

Hivi karibuni serikali ilitoa fedha kiasi cha shilingi million 38.45 kwa ajili ya ujenzi wa bweni la wanafunzi katika shule ya sekondari Chisenga na ujenzi wa vyoo katika shule ya msingi Kasote.

 

 

 

 

 

Comments