Viongozi wa Upinzani wakamatwa kwa kushinikiza maandamano

 


Baadhi ya viongozi wa upinzani nchini wanashikiliwa na polisi baada ya kutangaza kupanga maandamano ya amani siku ya Jumatatu ili kuonesha kutokubaliana na matokeo ya uchaguzi.

Polisi wanasema wamemkamata mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani Chadema bwana Freeman Mbowe pamoja na aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema na aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Ubungo Jijini Dar es Salaam Boniface Jacob.

Kamanda wa Polisi kanda maalumu ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa amesema walipiga marufuku maandamano hayo yaliyopangwa kuanza leo asubuhi, lakini viongozi wa Chadema "wameonekana kufanya vikao kuratibu maandamano ya fujo".

Amesema viongozi hayo walipanga kuhatarisha usalama wa raia kwa kwa kufanya vurugu kuonyesha kutokubaliana na matokeo, watu hao wanapanga kuingia mtaani kuchoma maeneo mbalimbali kama masoko, magari na vituo vya mafuta.

Aidha amesisitiza kuwa operesheni kubwa inaendelea kwa yeyote ambaye atashiriki kuratibu, kuwezesha au kushiriki katika maandamano hayo atafikishwa kwenye mikono ya sheria.

Baada ya rais John Magufuli kutangazwa kuwa rais kwa awamu ya pili siku ya Ijumaa usiku, viongozi wa vyama vikuu vya upinzani nchini Tanzania walitangaza kutokubaliana na matokeo hayo na kuitisha maandamano leo hii.

Comments