Mtendaji Aliewafungia Watoto Watoro Chumba kimoja Na Nguruwe Asimamishwa ‘’Nkasi’’


MKUU wa wilaya Nkasi mkoani Rukwa Said Mtanda ameagiza kusimamishwa kazi mara moja  kwa afisa mtendaji wa kijiji cha Matala Revocatus Tinga  kwa kosa la kuwakamata watoto watoro shuleni na kuwafungia chumba kimoja na Nguruwe.

Akizungumza na Wakazi wa kijiji cha Swahila mkuu huyo wa wilaya alidai kuwa yeye baada ya kupata taarifa hizo alimuagiza mkurugenzi mtendaji wa wilaya kumsimamisha kazi mtendaji huyo na kumpeleka mtendaji mwingine  katika kijiji hicho.

Alisema kuwa kitendo alichokifanya afisa mtendaji huyo hakikubaliki hivyo kwanza asimamishwe kazi na baada ya hapo akabidhiwe kwenye vyombo vya serikali kwa ajili ya uchunguzi.

Mkuu huyo wa wilaya alidai kuwa baada ya uchunguzi huo kukamilika na ikibainika kweli afisa mtendaji huyo amefanya kitendo hicho ataadhibiwa kwa mujibu wa sheria na mamlaka yake ya nidhamu.

“ni jambo lisilolokubalika kwa mtendaji wa kijiji ambaye ni mlinzi wa amani katika kijiji na anafanya kitendo hicho sisi kama serikali ni lazima tuchukue hatua stahiki”alisema mkuu wa wilaya

Sambamba na hilo aliwataka Wananchi wa kijiji  hicho kugawa muda wa kufanya kazi zao za kuandaa mashamba kuelekea msimu mwingine wa kilimo badala ya kukazana na masuala ya kisiasa katika kipindi hiki cha kampeni.

Alisema kuwa katika kipindi hiki ameshuhudia watu wengi wakijishughulisha na masuala ya kisiasa na kujikuta muda mwingi wakiutumia kwenye mambo ya kisiasa huku muda haumsubiri mtu na wasipoutumia muda huo vizuri msimu wa kilimo utafika na wao hawajajiandaa na mwisho wa siku ni kukumbwa na balaa la njaa.

Na aliwataka kuendelea kulinda amani katika kipindi hiki cha kampeni kuelekea uchaguzi mkuu ili ukifika wakati watu wenyewe watumie demokrasia kuweza kuwachagua viongozi bora wanaowataka wao.

Mwisho

Comments