Wazazi Waiomba Serikali Kutilia Mkazo Upimaji Ujauzito Kwa Wanafunzi.

katika picha  ni  katibu  tawala  wilayani  kalambo Frank  Sichalwe ,akiongea na viongozi katika  tarafa  ya kasanga

BAADHI ya wazazi wilayani Kalambo mkoani Rukwa wameiomba serikali kuanzisha mpango maalumu wa kuwapima ujauzito wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kila baada ya  miezi mitatu kama ilivyo  katika maeneo mengine ya mkoa huo ili kuwabaini walioanza kujihusisha na vitendo vya kimahusiano ya kingono na  wanaume  katika umri mdogo

Ombi hilo walilitoa kwa nyakati tofauti wakati wakizungumza na mwandishi wa habari hizi,muda mfupi baada ya kikao kazi kilichowakutanisha Katibu tawala wa wilaya hiyo  Frank Sichalwe pamoja na viongozi wa serikali za vijiji, kata pamoja na maofisa elimu kata waliopo katika maeneo ya mwambao wa ziwa Tanganyika.

Mmoja wa wazazi hao aliyejitambulisha kwa jina la Getruda Siwale mkazi wa kijiji cha Kasanga, alisema kuwa imefika wakati kwa serikali kutumia njia hiyo kwani tatizo la mimba za utotoni pamoja na kwa wanafunzi limekuwa ni changamoto kubwa hivyo ni lazima zibuniwe mbinu zitakazo sababisha wanafunzi  hao kuogopa kushiriki ngono.

Alisema kuwa nivema ukaanzishwa utaratibu wa kuwapima wanafunzi ujauzito kila baada ya  miezi mitatu kwani hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa  kupunguza mimba za utotoni ambazo zimekua zikisababisha wanafunzi wengi kukatisha masomo.

Mmoja wa wanafunzi anayesoma katika shule ya sekondari Matai,(jina limehifadhiwa) aliunga mkono ombi hilo,alisema kuwa iwapo mpango huo ukianza wanafunzi wengi wa kike wataacha kufanya ngono kwani wataingiwa na hofu .

Kwaupande wake katibu tawala wa wilaya hiyo, Frank Sichalwe aliwaonya baadhi ya wazazi ambao wamekuwa wakishindwa kutoa ushirikiano pindi Watoto wao ambao ni wanafunzi wanapopata ujauzito .

Alisema kuwa kitendo hicho ni kinyume na sheria hivyo watambue kuwa huenda wakajikuta wanafikishwa mahakamani lengo ni kuhakikisha kuwa wilaya hiyo inafanikiwa katika kukabiliana na mimba kwa wanafunzi.

Comments