Serikali Yatoa Tahadhari Ya Ugonjwa Wa Ebola.


Serikali  Yatoa Tahathari  Ya  Ugonjwa  Wa  Ebola.
WANANCHI  kutoka wilaya za Kalambo na Nkasi mkoani Rukwa wameiomba serikali  kuongeza vifaa  vya  kupimia  ugonjwa wa ebola pamoja na kutolewa elimu kutokana na wilaya hizo kuwa na mwingiliano mkubwa wa watu kutoka nchi jirani ya Congo na hivyo kuwa na hofu ya kuenezwa ugonjwa huo.
Wakiongea katika nyakati tofauti wananchi hao,walisema serikali haina  budi kudhibiti wahamiaji haramu kutoka nchi jirani ya Congo kutokana na ugonjwa huo kuripotiwa kuwepo nchini humo.
Wakiwa katika mkutano maalumu uliowajumuisha wataalamu wafya ngazi ya jamii na wadau mbalimbali katika wilaya za Nkasi na Kalambo wamedai kuwa mazingira ya ugonjwa huo ni hatarishi sana na hivyo vifaa vya kupimia ugonjwa huo vinatakiwa kwa wingi hasa kutokana na mwingiliano mkubwa uliopo kati ya Watanzania na Congo.
Lakini pia wizara ya afya imeshauliwa kuwatumia vyema Waganga wa jadi katika vita hii ya ugonjwa wa ebola kwani watu hao wakielimika vya kutosha watatoa msaada mkubwa kwa kuwaelekeza wateja wao kwenda hospitalini pale wanapobaini kuwa wateja wao wanaonesha dalili ya ugonjwa huo
Awali akitoa elimu kwa wananchi kutoka wilaya za Kalambo na Nkasi  mwakilishi kutoka wizara ya afya Ashole Mshana ,alisema serikali  imeanza kutoa tahadhari  kwa wananchi dhidi ya ugonjwa huo na kuwasihi wananchi hususani wanaoishi katika mwambao wa ziwa Tanganyika kuwa makini na wageni wanaoingia kwenye maeneo yao  husika  .

Mkuu wa wilaya ya kalambo mkoani humo Julieth Binyura alisema  lengo la serikali ni  kuhakikisha ugonjwa huo hauingii nchini.
Aidha  aliwasihi  wataalamu  kuendelea  kutoa  elimu kwa wananchi  juu  ya athari za ugonjwa  huo ikiwa  ni pamoja  na kuongeza vifaa  vya  kupimia ugonjwa huo haswa  kwa  wananchi  wanaoingia  kinyemera nchini kupitia njia za panya.

Comments