Katikati katika picha ni mkuu wa mkoa wa Rukwa Johim Wangabo akishiriki ujenzi wa vymba vya madarasa. |
Na Baraka Lusajo. Rukwa.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ametoa siku tano kwa
wazazi kuwaandikisha watoto waliofikisha umri wa kuanza shule pamoja na
kuwafikisha shuleni wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza
ambao kwa mwaka 2020 wanafunzi 16,062 wamechaguliwa kujiunga kidato cha kwanza
katika mkoa lakini hadi kufikia tarehe 24.1.2020 ni wanafunzi 11,149 pekee
wameripoti ambao ni sawa na asilimia 69.41.
Aidha, katika kuhakikisha asilimia 100 inafikiwa amewaagiza
watendaji wa Kata na vijiji mkoani humo kuwakamata na kuwashitaki kwa sheria ya
mtoto ya mwaka 2009 wazazi wasiofanya hivyo na kuongeza kuwa sheria hiyo ya
mtoto iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2016 inatamka wazi haki ya mtoto ikiwemo
haki ya kupata elimu na kwa mzazi kutofanya hivyo ni kosa na adhabu yake ni
kulipishwa faini au kufungwa jela ama vyote viwili kwa pamoja.
“Mimi natoa siku tano za wiki hii kwa wazazi wote ambao wana
watoto hawajaenda shule mpaka sasa hivi iwe ni wa darasa la kwanza, wawe ni
“form one” (kidato cha kwanza) baada ya siku hizi tano wakamatwe wafikishwe
mahakamani hatutaki mchezo kwenye elimu, huyu mtoto ukimchezea chezea hivi huyu
huyu ndio atatusumbua, kwasababu akitoroka shule anakimbia yamesmshinda ndio
huyo anakwenda mitaani, unadhani watoto wa mitaani wanatoka wapi si wameshindwa
shule huku, si wazaqzi wameshindwa kuwalea, wakamatwe wazazi wanashindwa
kuwalea watoto wao wafikishwe mahakamani, watendaji wa vijiji watendaji wa kata
kamateni wazazi hao” Alisisitiza.
Ameyasema hayo leo tarehe 27.1.2020 katika kikao kazi
kilichohudhuriwa na watendaji wa vijiji na kata za Halmashauri ya Wilaya ya
Sumbawanga pamoja na watumishi wa halmashauri hiyo walioongozwa na makamu
Mwenyekiti wa halmashauri pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga akianza ziara
yake ya siku nne ya kukagua idadi ya wanafunzi walioripoti shule pamoja na
mindombinu iliyopo.
Mh. Wangabo amesema kuwa mkoa kufanya vibaya kwenye elimu
kunachangiwa na kuchelewa kupeleka watoto shule na kuongeza kuwa endapo
tathmini inafanyika kwa wale wanaofanya vibaya kwenye mitihani yao utagundua ni
wale wanaochelewa kufika shule na kutahadharisha kuwa wanafunzi wa
kidato cha kwanza wapo katika kipindi cha mabadiliko kutoka kwenye ufundishwaji
wa Kiswahili kwenda kwenye ufundishwaji wa kiingereza hivyo ni muhimu kwao
kuwahi shuleni.
“Anatoka mazingira ya shule ya msingi anaingia ya sekondari ,
inapaswa mwanafunzi wa “form one” aanze mapema hata kabla ya shule kufunguliwa
ili aaanze kuzoea zoea yale mazingira lakini hajafika mapema, shule
imefunguliwa hayupo, mwezi mzima unapita hayupo shuleni , huyu hata “form two”
unategemea atafaulu kweli?” Alihoji.
Halikadhalika, Mh. Wangabo amewataka watendaji hao kushirikiana
na wenyeviti wa vijiji kuitisha mikutano ya vijiji na kuwaelimisha wazazi
juu ya umuhimu kumuwahisha mtoto mapema shuleni huku wakiwabainishia
faida na hasara za kutofanya hivyo na kuwaeleza juu ya umuhimu wa kusomesha
watoto kwa maendeleo ya mkoa na nchi kwa ujumla.
Wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza kwa
Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ni 4,394 huku walioripoti ni wanafunzi
2,973 ambao ni sawa na asilimia 67.7 huku wakihitaji madarasa 18 ambapo
madarasa 15 tayari yamefikia usawa wa linta huku Mh Wangabo akitoa ahadi
ya kuchangia mifuko ya saruji 150 ili kuwezesha kukamilisha ujenzi wa
madarasa hayo.
Comments
Post a Comment