WAKAZI wa Kijiji cha Samazi wilayani Kalambo
mkoani Rukwa wamelalamikia kucheleweshwa
kwa ujenzi wa kituo
cha afya ambacho
kilitakiwa kujengwa tangia june 2019 kutokana na fedha
kutolewa na serikali kiasi cha shilingi million 400 na hivyo
kuwa na hofu ya
fedha hizo kuhamishwa.
Malalamiko hayo waliyatoa mbele ya Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Dorothy
Gwajima alipofanya ziara ya kikazi wilayani humo na kutembelea eneo
linalojengwa kituo hicho cha afya.
Mmoja wa wakazi wa Kijiji hicho Saimon Kapesa
alisema kuwa kutokana na kukosekana kwa kituo cha afya katika kata yao,wanalazimika
kutembea umbali wa zaidi ya kilometa 20 kutafuta huduma za afya katika kata
nyingine hivyo waliiomba serikali iwajengee kutuo hicho cha afya haraka ili kuwaondolea
usumbufu.
"Katika Kijiji chetu, tunalazimika
kutembea umbali wa zaidi ya kilometa 20 kutafuta huduma za afya, na hii ni tabu
zaidi kwa akina mama wajawazito na watoto ambapo wakati mwingine wanahitaji
huduma za dharura na pengine hata baadhi ya vifo vinavyotokea kijijini hapa
vinatokana na kukosekana kwa matibabu kwa wakati" alisema.
Naye Monica Nakazwe mkazi wa Kijiji hicho
alisema kuwa haoni sababu kwanini kuna kusua sua katika ujenzi wa kituo hicho ilihali
serikali imekwisha toa fedha kwaajili ya ujenzi wa kituo hicho kwani kwa
kufanya hivyo kunawasababishia usumbufu na gharama zisizokuwa za lazima katika
kufuata huduma za afya katika vituo vya afya vya Ngorotwa na Matai, ambavyo
vipo mbali na kijiji chao.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri
ya Wilaya ya Kalambo, Nicholaus Mlango alisema kuwa ni kweli serikali imetoa
fedha kiasi cha shilingi milioni 400 na tayari halmashauri hiyo imekwisha anza
ujenzi wa kituo hicho cha afya.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kalambo, Frank
Sichalwe aliishukuru serikali kwa kutoa
fedha hizo ambapo tayari ujenzi wa kituo cha afya umekwisha anza na utakapo
kamikika utaondoa kero zinazo wakabili wakazi wa kijiji hicho.
Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI, Gwajima alitishia kuzichukua fedha
hizo kiasi cha shilingi milioni 400 zilizotolewa na serikali kwaajili ya ujenzi
wa kituo cha afya cha samazi, huku akimpa siku saba Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kalambo kuanza mara moja
ujenzi wa kituo hicho ambacho umeshindwa kuanza kwa takribani miezi minane
kutokana na mvutano wa eneo la ujenzi.
Comments
Post a Comment