Katika picha ni mkuu wa mkoa wa Rukwa akimpatia zawadi ya fedha mmoja wa wenyeviti wa serikali za vijiji baada ya kushinda . |
Na Baraka Lusajo. Kalambo
Viongozi
wapya 2,766 wa vijiji na vitongoji walioshinda katika uchaguzi wa serikali
za mitaa uliofanyika tarehe 24.11.2019 katika wilaya ya Kalambo wametakiwa
kuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanatatua kero na malalamiko ya wananchi
wanaowahudumia katika vijiji na vitongoji ili kupunguza msongamano wa wananchi
wanaohitaji kutatuliwa kero zao katika ngazi ya wilaya na mkoa.
Hayo
yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo muda mfupi baada ya
viongozi hao kula kiapo mbele yake na mbele hakimu wa mahakama ya Wilaya ya
Kalambo ambapo wenyeviti wa vijiji na vitongoji kutoka katika kata 10 za tarafa
ya Matai wilayani humo walishiriki katika kiapo hicho.
“Katika
ngazi hiyo ya vijiji, vitongoji na mitaa, wenyeviti wa maeneo hayo mimi
nikipata mtu anatoka kwenye vijiji vyenu analalamika kwa jambo ambalo ni dogo
sana, nitakuita. Utapata usumbufu wa kuja Sumbawanga, uhesabu kuwa utatumia
gharama zako kuja na kurudi kutoka kule kwenye kijiji chako. Nitakusumbua
kwasababu wewe hutaki kusumbuka nikilipata tu nitakusumbua, kwahiyo nendeni
mkatatue kero za wananchi katika ngazi zenu, yako mambo mengi mtusaidie sio
kila kitu mkuu wa mkoa, kila kitu mkuu wa Wilaya na wengine wanakwenda
wanaandika mpaka kwa Rais,”Alisisitiza.
katika picha ni baadhi ya wenyeviti wa serikali za vijiji wakiapishwa |
Aidha
amewataka viongozi hao kuwatumikia wananchi wote bila ya kujali vyama vyao vya
kisiasa, dini wala kabila na kuwataka katika utekelezaji huo kuwa shirikisha
kwani wasipofanya hivyo wananchi watashindwa kushiriki katika shughuli za
kimaendeleo jambo litakalorudisha nyuma juhudi za mkoa kuhakikisha wananchi
wake wanapata huduma stahiki na kwa wakati.
“Mambo
ambayo mnapaswa kwenda kuyasimamia katika maeneo yenu kuwashirikisha wananchi
katika kupanga maendeleo, sio unakurupuka tu unasema mimi nataka hiki kifanyike
bila ya kuwashirikisha wananchi , lazima wapange waamue wao wenyewe na
wakishaamua wao wenyewe watashiriki katika kutekeleza lakini pia watasimamia
kulinda yale maamuzi yao na hiyo ndio demokrasia na hili ndilo mkalifanye kule,
viongozi wengine wakishachaguliwa kama hivi wanakuwa miungu watu, hatupendi
kuona miungu watu kwenye vijiji vitongoji na mitaa,” Alisema.
Katika picha ni mkuu wa mkoa akisalimiana na viongozi wa serikali za vijiji mara baada ya kuapishwa. |
Na katika kuhakikisha viongozi hao wanatekeleza majukumu yao bila ya visingizio amewaagiza wakurugenzi wote wa halmashauri nne za mkoa huo kuwapatia mafunzo viongozi hao wapya pamoja na wale ambao ni muhula wao wa pili au zaidi jambao litakalo wasaidia kutekeleza majukumu yao kwa Mujibu wa Sera za Kisekta, Mikakati ya Kisekta, Sheria, Kanuni, Miongozo na Taratibu zinazosimamia Sekta husika.
Wakati akitoa muhtasari
wa taarifa ya uchaguzi wa serikali za mitaa mratibu wa uchaguzi mkoa Albinus
Mgonya alisema kuwa mitaa 165 iliyopo katika Manispaa ya Sumbawanga
imechukuliwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) ambayo ni sawa na asilimia 100 wakati
katika ngazi ya vijiji CCM imechukua vijiji 336 huku Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) kikichukua vijiji 2 kati ya vijiji 339 vya mkoa wa Rukwa.
“Vitongoji
vilivyoshiriki katika uchaguzi ni 1,816 na kwa nafasi ya vitongoji Chama cha
Mapinduzi kimepata nafasi 1,807 sawa na asilimia 99.4 Chama cha Demokrasia na
Maendeleo kimepata nafasi za wenyeviti wa vitongoji 8 sawa na asilimia 0.6. kwa
faida ya wadau waliopo hapa nafasi hizi 8 mgawanyo wake ni kama ifuatavyo,
Sumbawanga Manispaa nafasi 1, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga nafasi 1 na
Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi nafasi 6,” Alimalizia.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo Mh. Daudi Sichone
wakati akitoa neno la shukurani aliwataka viongozi hao wapya kuhakikisha
wanawapatia elimu ya kutosha wananchi wanaowaongoza juu ya kutatua kero na
malalamiko katika ngazi hizo zao na sio kumshawishi mwananchi afike ngazi mkoa.
“Hawa
viongozi wetu wanatumia mkoa na taifa, hebu ifike mahali tutoe elimu kwa
wananchi wetu, kabla hajafika huko angalau akifika kule ionekane sisi sote
tunasapoti kwamba kwa tatizo lako hili ni vyema ukafika kwa mkuu wa mkoa lakini
sio tu unaamka tu na masimu yako unamuhangaisha mzee wa watu anashindwa kufanya
kazi za watu,”Alisema.
Maeneo
yaliyofanya uchaguzi katika mkoa wa Rukwa ni vijiji 67, vitongoji 348, mitaa 9
na wananchi walioshiriki kupiga kura ni 118,887 huku zoezi hilo la uchaguzi
likiwa limefanyika katika hali ya amani na utulivu.
Comments
Post a Comment