Na Mwandishi wetu- Rukwa
Jeshi
la polisi wilayani Kalambo mkoani Rukwa
inamshikilia mwalimu wa shule ya msingi Kisumba(jina limehifadhiwa) mwenye umri
wa miaka 31 kwa tuhuma za kumpa mimba mwanafunzi wa shule ya sekondari Chisenga
iliyopo wilayani humo.
Kwamujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kamanda wa polisi mkoani
humo Justine Masejo ilieleza kuwa mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 18
alikuwa anasoma kidato cha kwanza katika shule hiyo.
Alisema kuwa mtuhumiwa huyo anadaiwa kuwa alikuwa na uhusiano wa
kimapenzi na mwanafunzi huyo hadi kupelekea kumpa ujauzito.
Kamanda Masejo alisema kuwa mpaka sasa mkoani humo kuna jumla ya
matukio 27 yaliyoripotiwa katika vituo mbalimbali vya polisi ambayo
yanahusiana na wanafunzi kukatisha masomo baada ya kupewa ujauzito.
Alisema kuwa katika kesi hizo wanafunzi 20 ni wa shule za
sekondari na saba ni shule za msingi na zipo katika hatua mbalimbali za
upelelezi huku baadhi zimekwisha fikishwa mahakamani.
Kamanda huyo wa polisi alisema kuwa hivi sasa jeshi hilo la
polisi lina endesha operesheni maalum ya kuwakamata watu wanaojihusisha na
vitendo vya mapenzi na wanafunzi kwani wamekuwa ni kikwazo cha utekelezaji wa
nia njema ya serikali ya kutoa elimu bila malipo ili wanafunzi wengi waweze
kusoma mkoani Rukwa.
Alisema katika tukio hilo lililotokea hivi karibuni bado polisi
wanaendelea na upelelezi na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara tu upelelezi
utakapo kamilika.
Comments
Post a Comment