Mtoto Afariki Dunia Na Wengine 30 Kupatiwa Matibabu Baada Ya Kula Mzoga Wa Nguruwe



Na  Baraka   Lusajo. Kalambo

MTOTO Maren Namsukuma (7) amefariki dunia na watu wengine 30 wamepata matibabu  katika zahanati ya Kalembe Kijiji cha Utengule kata ya Mambwe Nkoswe wilayani Kalambo mkoani Rukwa baada ya kula mzoga wa nguruwe.

Kwamujibu wa taarifa ya kamanda wa polisi mkoani Rukwa Justine Masejo ilisema kuwa siku ya Desemba 21 Osward Simpungwe alichinja nguruwe ambaye alikuwa amekufua mwenyewe na kisha kuanza kuuza nyama.

Wakazi wa kijiji hicho akiwemo baba wa marehemu walinunua nyama hiyo na kuitumia kwaajili ya kitoweo, ndipo waliokula nyama hiyo walianza kuugua ugonjwa ambao haukujulikana mara moja.

Kabla ya kufariki mtoto huyo familia nzima walilalamika kuumwa tumbo, ndipo baba yao alipokwenda kwenye duka la dawa muhimu za binaadamu na kununua Flagyl pamoja na Panadol na kumpatia mtoto huyo,lakini hata hivyo hazikumsaidia na hali yake ilizidi kuwa mbaya na ilipofika majira ya saa 10 usiku siku ya Desemba 25, alifariki dunia wakati wakienda katika zahanati ya Kijiji kupata matibabu.
Mmoja wa wakazi wakazi wa Kijiji hicho aliyenusurika baada ya  kula nyama hiyo, Aberi Sinyangwe alisema kuwa katika Kijiji hicho kumekuwa na  changamoto  ya  kutokea matukio hayo kutokana na kukosekana kwa  maafisa  mifugo ambao wanajukumu la kukagua ubora wa nyama kabla ya kuliwa na binaadamu.

Aliiomba serikali  kupeleka wataalamu  hao kwa ili waondokane  na tatizo la kujirudia  kwa  matukio hayo.

Mwenyekiti wa kijiji hicho Wigani Namsukuma alisema kuwa baada ya serikali ya kijiji kupata taarifa za tukio hilo ilitoa taarifa polisi na kisha kuwakimbiza katika zahanati ya Kijiji wagonjwa 30 waliougua baada ya kula nyama hiyo na walipatiwa matibabu lakini kwa bahati mbaya alifariki mtoto huyo. 


Naye ofisa mifugo wa  wilaya ya Kalambo, Enos Luvinga aliwaonya wakazi wa Kijiji hicho kuacha tabia ya  kula  nyama za mifugo inayo jifia yenyewe kwani ni hatari kwa afya zao kwakua mifugo hiyo inakuwa na magonjwa ndiyo maana inajifia yenyewe.

Kaimu Mganga mkuu was wilaya ya Kalambo Rock Sabuni aliwashauri wakazi wa kijiji hicho kuacha tabia ya kujinunulia dawa na kutumia bila kupata ushauri wa daktari, badala yake wanapougua wawe wanakwenda haraka katika zahanati na vituo vya afya kwaajili ya matibabu.

Kamanda Masejo alisema kuwa Simpungwe anashikiliwa na polisi kwa mahojiano kutokana na kosa la kuwauzia watu nyama ya mzoga huo na atafikishwa mahakamani baada ya mahojiano hayo kukamilika.

Comments


  1. Ni hatari sana kula mizoga iliyojifia. Mabadiliko yanahitajika, na yanaanzia kwako wewe mwananchi!. Chukua hatua, okoa maisha yako na ya jamii yako!

    ReplyDelete

Post a Comment