Katika picha ni mkuu wa mkoa wa Rukwa Joachim Wangabo. |
Na Baraka Lusajo. Rukwa.
MKUU wa mkoa wa Rukwa Joachim
Wangabo ameziagiza Halmashauri mkoani
humo kuhakikisha zinakamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa 2888 ili wanafunzi
waliokosa nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza waweze kwenda Sekondari.
Agizo hilo alilitoa jana wakati akifungua kikao cha kamati ya ushauri
mkoa wa Rukwa(RCC) katika mwaka wa fedha 2019/2020 kilichofanyika katika ukumbi
uliopo katika jengo la ofisi ya mkuu wa mkoa huo.
Alisema kuwa wanafunzi Waliofaulu darasa la saba mwaka 2019
ni 16,069,kati ya hao wavulana ni 7,953 na Wasichana ni 8,116, na nafasi
zilizopo ni 13,128.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa Wanafunzi ambao watakosa nafasi
katika Halmashauri ya wilaya ya Kalambo ni 361,wilaya ya Nkasi Wanafunzi
1554, wilaya ya Sumbawanga Manispaa ni Wanafunzi 179 na Halmashauri ya Wilaya
ya Sumbawanga ni Wanafunzi 794.
Kutokana na takwimu hizo Halmashauri ya Nkasi inaongoza kwa kuwa
na Wanafunzi wengi watakao kosa nafasi ikifuatiwa na Halmashauri ya Sumbawanga,
Kalambo na Halmashauri ya Manispaa.
Aidha Wangabo aliwaagiza wakuu wa wilaya za mkoa huo kuhakikisha
kuwa wanafunzi wote waliofaulu wanajiunga kidato cha kwanza ifikapo Januari
2020 na kuwa hakutakuwa na udahili wa pili wanafunzi wa kidato cha kwanza
kwa mwaka 2020.
Katika kikao hicho mbunge wa mkoa huo wa Rukwa Silafi Maufi
alishauri kuwepo na kawaida ya kuwapima mimba wanafunzi mara kwa mara kuliko
kusubilia mpaka ahisiwe mwanafunzi kuwa na ujauzito na wanaume walio sababisha
mimba hizo wakamatwe na kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo mkoa huo wa Rukwa unajumla ya wanafunzi 294
waliokatisha masomo kutokana na kupata ujauzito katika kipindi cha mwaka huu wa
2019.
Mwisho
Comments
Post a Comment