Uchaguzi Wa Mitaa Uliosusiwa Na Wapinzani Wafanyika Huku Baadhi Ya Maeneo Wagombea Wa CCM Wakipita Bila kupingwa
KATIKA PICHA NI MSIMAMIZI WA UCHAGUZI WILAYANI KALAMBO ERICK KAYOMBO |
Wakazi wa wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa wamejitokeza kupiga kura,
asubuhi ya siku ya Jumapili, huku ulinzi ukiwa umeimarishwa tangu kuanza kwa
zoezi la kupiga kura.
Hata hivyo katika
maeneo kadhaa zoezi likionekana kwenda vizuri , huku kwenye maeneo mengine
zoezi halikufanyika kabisa kwa kile kilichoelezwa kuwa kulikuwa na mgombea
mmoja tu ambaye amepita bila kupingwa.
Mfano katika wilaya ya
Kalambo ambayo ilikuwa na vijiji 33 na
vitongoji 78 vinayowaniwa, katika maeneo
mengi wagombea wa chama cha CCM
walipita bila kupingwa katika nafasi zote, isipokuwa katika vitongoji vitano pekee ,kwa mujibu wa Msimamizi wa uchaguzi wilayani Kalambo Elick Kayombo.
Hata hivyo pamoja na
viongozi wakuu wa vyama vya upinzani kutangaza kususia uchaguzi huo, lakini
wagombea wa baadhi ya vyama hivyo waliendelea kuwania nafasi mbalimbali katika
baadhi ya maeneo wilayani humo.
Uchaguzi huu hufanyika
chini ya Ibara ya 8 (1) (a) ya Katiba ya Tanzania kuwa ni nchi inayofuata
misingi ya demokrasia na haki ya kijamii na kuwa ndiyo msingi wa mamlaka yote
iliyonayo serikali hupata kutoka kwa wananchi.
Vyama vilivyotangaza
kujitoa kushiriki kinyang'nyiro cha uchaguzi huo ni Chadema, UMD, CCK,
NCCR-Mageuzi, NLD, ACT-Wazalendo, CUF na Chauma.
Licha ya Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Seleman
Jaffo, mwenye dhamana ya uchaguzi huo kutoa matamko mawili yenye nia ya
kuviomba vyama vya upinzani kulegeza misimamo yao na kuwataka wagombea
walioteuliwa kuendelea na uchaguzi huo, lakini hapakuwa na mafanikio yoyote.
Katika taarifa yake
iliyokaririwa na vyombo vya habari nchini,Waziri Jaffo alivikosoa pia vyama vya
siasa kwa kile alichokiita kushindwa kuwaelekeza wagombea wao namna nzuri ya
kujaza fomu za kuomba kuteuliwa katika nafasi wanazogombea kwenye mitaa, vitongoji
na vijiji.
"Inaonesha vyama
vya siasa vilishindwa kuwasimamia wagombea wao wakati wa kujaza fomu hizo, kwa
maana makosa mengine yalionekana ni kama ya mtu alijaza ili kushindwa
mapema." Hilo alilitoa wakati anazungumzia suala la vyama vya siasa kujitoa
kwenye uchaguzi huo, lakini vyama vilivyojitoa vilisimama kidete na kupinga
mchakato mzima wa uchaguzi.
Comments
Post a Comment