WAKULIMA WAIOMBA SERIKALI KUSAMBAZA PEMBEJEO ZA KILIMO KABLA YA MSIMU KUANZA.



 Na  Baraka  Lusajo.
Wakulima wilayani Kalambo mkoani Rukwa wamelalamikia kukosekana kwa pembejeo pamoja na bei elekezi katika msimu huu wa kilimo hali inayotia hofu kutopata mavuno kutokana na wakulima wengi kulima bila kutumia pembejeo.
Mmoja wa wakulima hao Samu Mwasomola, alisema kuwa kumekuwepo na changamoto ya upatikanaji wa pembejeo za kilimo kitendo kinachopelekea wakulima  kutumia  mbegu  zisizo faa na zisizo na ubora.
Naye Edwini Mwasabwite,alisema kuwa wanaiomba serikali kuwa na mazoea ya kuwahisha  pembejeo  za kilimo  kabla ya msimu kuanza  kwa lengo la kuwawezesha wakulima kupata  mazao mengi na kuondokana na adha ya kutumia  pembejeo zisizo na ubora.
Naye kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kalambo Nikoraus Mrango, alisema kuwa serikali imesambaza  pembejeo za kilimo katika  maduka  yote yanayouza pembejeo sambamba na kutoa bei elekezi.
Alisema kuwa kinachofanyika hivi sasa  ni kukagua kama pembejeo hizo  zinawafikia  wakulima na kuwataka wakulima  kutoa taarifa  endapo kuna changamoto  zinazowakabili katika maeneo  yao husika.
‘’tutachukua hatua kali  kwa  mujibu  wa  sheria  endapo  kuna wauzaji  wa  pembejeo  watakao bainika kukiuka taratibu wakati wa kuwauzia  pembejeo wakulima’’alisema Mrango.
Awali akiongea  kupitia madhimisho ya msimu wa  kilimo  Julieth Binyura  aliwataka  watendaji wa Halmashauri hiyo kusimamia  na kuhakikisha  wauzaji   wa pembejeo  wanauza pembejeo  za kilimo  kwa  bei  elekezi.
Pia alisema wilaya inaendelea kusisiza wakulima kulima kibiashara mazao mbalimbali ikiwemo Alizeti na kahawa ili  kuongeza  wigo wa mazao yanalimwa  na  kupunguza utegemezi kwenye  zao la mahindi ambalo wakati mwingie bei yake imekuwa haitabiliki.
Hivi karibuni mkoa wa Rukwa ulizindua msimu mpya wa kilimo kwa mwaka 2019/20 na unakusudia kulima hekta 603,637.13 za mazao mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wanakuwa na uhakika wa chakula.
Mwisho


Comments