Papa Francis atoa wito wa kupigwa marufuku kwa silaha za nyuklia duniani.

Papa Francis alifanya ibada katika eneo la mkasa wa bomu la kinyuklia wakati wa ziara hiyo.Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis amewasilisha ombi la kupigwa marufuku kwa silaha za kinyuklia wakati wa ziara yake ya Nagasaki , mojawapo ya miji miwili ya Japan iliyoshambuliwa na mabomu ya kinyuklia wakati wa vita vya dunia vya pili.
Alilalamikia uwepo wa silaha za kinyuklia akisema kwamba sio suluhu ya amani duniani.
Takriban watu 74,000 waliuawa kufuatia shambulio la Nagasaki lililotekelezwa na vikosi vya Marekani 1945.
Manusura wawili wa bomu hilo , wote wakiwa na umri wa miaka 45 waliwasilisha shada lao la maua kwa papa Francis wakati wa ibada hiyo ya Jumapili.
Papa Francis aliwasili kutoka Thailand siku ya Jumamosi kwa ziara ya siku nne akiwa papa wa pili kutembelea Japan.
Mamia ya wafuasi wa kanisa katoliki walikusanyika wakati ambapo mvua ilikuwa ikinyesha katika mji wa Nagasaki.
Papa Francis baadaye alihudhuria mkutano katika eneo la kumbukumbu za Hiroshima ,eneo la shambulio la bomu la atomiki.

Je Papa Francis alisemaje?

Katika sherehe hiyo iliojaa huzuni, papa Francis alishutumu matumizi ya silaha za kinyuklia.
''Eneo hili linatukumbusha uchungu na hatari ambayo sisi wanadamu tunaweza kufanyia wengine'', alisema katika hafla hiyo ya Nagasaki.
Wakati wa hotuba yake , Papa Francis alizungumzia kuhusu matumizi yake akisema kuwa amani haitapatikana kukiwa na hofu ya kutaka kuangamizana ama hofu ya uharibifu.
Pia alikosoa fedha zilizotumika kununua silaha duniani na kuzungumzia kuhusu mazingira ya kutoaminiana swala linalosababisha kusambaa kwa silaha ndogo ndogo.
Sakue Shimohira mwenye umri wa miaka 85 na Shigemi Fukahoi mwenye umri wa miaka 89 ni manusura wawili waliokutana na Papa Francis wakati wa ziara hiyo.
''Mamangu na dadangu mkubwa waliuawa'' , bi Shimohira alinukuliwa na chombo cha habari cha AFP akisema. Hata iwapo ulinusurika, hauwezi kuishi kama binadamu ....Hilo ndio tishio la silaha za kinyuklia.
Ziara hiyo ni ya kwanza kwa Papa katika kipindi cha miaka 38Haki miliki ya pichaAFP
Image captionZiara hiyo ni ya kwanza kwa Papa katika kipindi cha miaka 38
Nagasaki ni maarufu kwa kuwa nyumbani kwa Wakristo waliojificha ambao hufanya ibada yao kwa kujificha wakati dini yao ilipopigwa marufuku karne ya 17.

Ni nini haswa kilichotokea Hiroshima na Nagasaki?

Bomu la kwanza la kinyuklia liliangushwa katika mji huo na ndege ya Marekani tarehe 6 Agosti 1945.
Marekani ilitumai kwamba bomu hilo lililorushwa baada ya Japan kukataa ombi la awali la amani litailazimu nchi hiyo kusalimu amri bila wanajeshi wa Marekani kupata majeraha yoyote katika makabiliano ardhini.
Bomu la kwanza liliwaua takriban watu 140,000 mjini Hiroshima - huku nusu ya idadi hiyo wakiaminika kufariki papo hapo wakati bomu hilo lilipoanguka.
Maelfu waliuawa papo hapo mjini Nagasaki mnamo tarahe 9 Agosti 1945Haki miliki ya pichaCORBIS VIA GETTY IMAGES
Image captionMaelfu waliuawa papo hapo mjini Nagasaki mnamo tarahe 9 Agosti 1945
Shambulo hilo ndilo lililokuwa la kwanza la matumizi ya silaha za kinyuklia ambayo ilikuwa imeundwa wakati wa vita.
Rais wa Marekani Harry Truman alitangaza kuhusu uwepo wa silaha hiyo baada ya bomu la kwanza kuangushwa.
Baada ya Japan kukataa kusalimu amri , wanajeshi wa Marekani waliangusha bomu la pili siku tatu baadaye.
Nagasaki sio mji uliolengwa katika shambulio hilo lakini ulichaguliwa baada ya hali mbaya ya hewa kukumba mji wa Kokura.
Japan ilisalimu amri siku sita baadaye hatua iliositisha vita vya dunia vya pili.
Uwepo wa bomu hilo na uharibifu wake na athari zake umepingwa sana tangu wakati huo.

Comments