Kiongozi wa kijiji athibitisha tukio la mama kumuua na kumla mwanae

Mama amuua mwanaeKumradhi baadhi yenu mnaweza kuona taarifa hii kuwa ya kuogofya

Huenda likawa ni jambo lenye ukakasi kwenye masikio, lakini tukio la kushangaza limetokea katika mkoa wa Njombe Nyanda za Juu kusini mwa Tanzania baada ya mwanamke mmoja kumchinja mwanae wa miaka minne na kisha kula baadhi ya viungo vyake huku vingine vikipotelea porini.
Diwani wa kata ya Mavanga eneo la Ludewa mkoani Njombe, bwana Emmanuel Ngalalikwa anasimulia kile kilichotokea:
"Baba wa familia ile alienda shambani kama kilomita kumi na mama ndiye alibaki peke yake nyumbani.
Na ndio wakati ambao inadaiwa kuwa alimuua mwanae.
Tukio hilo linadaiwa kufanyika kati ya siku ya Ijumaa au Jumamosi na liligundulika baada ya mume wake kurudi nyumbani kutoka shambani siku ya jumapili saa 12 jioni.
Mume wake aliporejea nyumbani alimkuta mtoto mmoja tu nyumbani na alipomuuliza mke wake mtoto mwingine yuko wapi? akajibiwa kuwa anatakiwa kwenda kulipa mahari akiwa anamaanisha kupeleka ng'ombe na mbuzi kwao.
Vilevile mke alidai kuwa alimwambia mume wake muda mrefu kumpeleka kwa wazazi wake lakini hakutaka kwenda kwa hiyo hana mamlaka ya kumuuliza mtoto yuko wapi
Baada ya siku moja, majirani na viongozi wa serikali ya kijiji walichukua jukumu la kumuhoji yule mama, kujua mtoto yuko wapi.
Na mama hakuwa mzito kujieleza na kudai kuwa mtoto amemuua yeye mwenyewe na mume wake hana mamlaka ya kumuhoji mtoto yuko wapi.
Mama huyo alikiri kumuua, kumpika na kumla mwanawe kichakani.
Tukio hilo lilitokea wakati mtoto wake mkubwa wa kiume ambaye anasoma darasa la pili alikuwa ameenda kwa babu yake.
Uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea.
Mpaka sasa mtuhumiwa Christina Mlelwa pamoja na mume wake wanashikiliwa na polisi .
Haijathibitishwa iwapo mama huyo ana tatizo la afya ya akili ama la.
Kwa mujibu wa diwani Ngalalikwa miaka miwili iliyopita mama huyo aliwahi kumshambulia mtoto wake kwa kumn'gata meno.
Mabaki yaliyopatikana ni fuvu la kichwa ambalo liko kituo cha polisi, na mabaki mengine bado yanatafutwa.
HANZO  CHA  HABARI BBC SWAHILI

Comments