Kesi ya Mwandishi Eric Kabendera yasubiri hakimu mpya

Eric Kabendera (kulia)Kesi ya mwandishi mashuhuri wa habari za kiuchunguzi wa Tanzania Erick Kabendera imeahirishwa tena hadi tarehe 20 Novemba.
Sababu ya kuahirishwa kwa kesi hiyo leo imetajwa kuwa ni kusubiri kuteuliwa kwa hakimu mpya.
Hakimu Augustine Rwezile, ambaye ndiye alikuwa anasikiliza kesi ya Kabendera hivi karibuni aliteuliwa kuwa jaji wa Mahakama Kuu.
Kesi ya Kabendera imeahirishwa mara kadhaa sasa, huko nyuma upande wa mashitaka ukisema sababu ni kutokukamilika kwa upelelezi wa kesi hiyo.
Mwandishi huyu wa habari anatuhumiwa kutokulipa kodi, kutakatisha fedha na kutoa msaada katika genge la uhalifu.
Kabendera amekana tuhuma zote hizi.
Unaweza kusoma pia:
Mwezi Septemba mwaka huu, Rais John Magufuli alimshauri Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Biswalo Mganga kufungua majadiliano hasa na mahabusu wa makosa mbalimbali hasa ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha ambao wako tayari kuomba msamahama na kurudisha fedha
Kabendera amekubali kuingia katika majadiliano haya na DPP, mchakato ambao bado unaendelea.
Kabendera alishtakiwa mwezi Agosti kwa kosa la kupanga uhalifu, kushindwa kulipa kodi na kutakatisha fedha.
Wakili wa mwandishi huyo wa habari alimuomba rais John Pombe Magufuli amsamehe mteja wake , ambaye anasema hana hatia.
''Kufanya kazi kama mwandishi wa habari ni changamoto na kama Kabendera kwa kiasi fulani alikosea , tunaomba msamaha. Kama rais anasikia hili , kwa unyenyekevu tunuomba kulingalia hili na kama mawakili tuko tayari kufanya kitu kinachohitajika kumuwezesha kuwa huru,'' Wakili Jebra Kambole aliwaambia waandishi wa habari.

Comments