Na Baraka Lusajo.Rukwa
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa
Mh. Joachim Wangabo amekabidhi watumishi 42 wa halmashauri ya Wilaya ya
Sumbawanga pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kwa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa mkoani Rukwa kwa uchunguzi wa upotevu wa fedha wa zaidi ya
shilingi milioni 916 baada ya kuonekana utetezi wao juu ya upotevu wa fedha
hizo kutokuwa na vielelezo vya kutosha.
Mh. Wangabo ametoa maelekezo hayo baada ya kuitisha kikao cha
Wakurugenzi, Wawekahazina, wahasibu na watendaji wa vijiji na kata wa
halmashauri zote nne mkoani hapa ambao mfumo wa ukusanyaji mapato ngazi ya
halmashauri (Local Government Revenue Collection Information System – LGRCIS)
kuonesha kuwa fedha za makusanyo yao kubaki mifukoni mwao.
Aidha, Ametoa siku saba kwa wale wote ambao hawajawasilisha
fedha za makusanyo yao benki kuhakikisha wanawasilisha fedha hizo ikiwemo wale
waliokabidhiwa kwa TAKUKURU na kuonya kuwa endapo fedha hizo hazitawasilishwa
kesi hiyo itatoka TAKUKURU na Kuhamia Jeshi la Polisi ili kuwafikisha
mahakamani.
“Mimi natafuta fedha
ukishindikana tutakufunga, na ndio maana nimesema jambo hili kwanza
lishughulikiwe kwanza na TAKUKURU mpaka uturudishie hizo fedha kwa muda maalum
ambao nimeutoa, nimeshatoa siku sita zimeisha leo hii natoa siku saba nyingine,
wacha hawa ambao watakuwa wamerudisha, wale ambao watakuwa hawajakabidhisha
fedha zao, nitatoa siku saba baada ya hapo kesi hii itatoka TAKUKURU na kuhamia
polisi ili iende mahakamani,” Alisema
Katika kujadili sababu mbalimbali zinazopelekea fedha za
makusanyo kutumiwa bila ya utaratibu maalum mkaguzi wa ndani wa Halmashauri ya
Wilaya ya Nkasi Joseph Sengerema amesema kuwa matatizo ya upotevu wa fedha hizo
yanasababishwa kutokana na kukiuka sheria ya fedha za Serikali za Mitaa ambayo
hairuhusu Mtendaji kufanya matumizi yoyote bila ya ridhaa ya mkurugenzi wa
Halmashuri na kabla ya kuwasilisha fedha hizo benki.
“ Ukiangalia katika Halmashuri ya Wilya ya Nkasi mimi
nishatahadharisha kwamba, kuna hatari kubwa mtendaji wa kijiji anapokusanya
fedha halafu anapeleka fedha hiyo kwa mtendaji wa kata bila ya kuwa na nyaraka
maalum inayokiri upokezi wa fedha hizo, kwa hali hiyo unawezaje kusimamia ili
fedha hizi zisipotee? Na pia mtendaji wa kata anapozifikisha idara ya fedha
anahakikishaje zinfishwa benki kwa wakati?” Alihoji.
Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda
limshukuru Mh. Wangabo kwa kuwasaidia kupambana na upotevu wa mapato katika
halmashauri jambo ambalo wamekuwa wakilitolea maelekezo akiwa na kamati ya
ulinzi na usalama ya wilaya bila ya matunda.
“Usikivu wa watendaji wetu ni mdogo sana lakini nikuahidi kwamba
maelekezo uliyoyatoa ya siku saba nitayafanyia kazi na kesho Defaulters
(wadaiwa) wote tukutane pale ukumbi mdogo wa halmashauri ili niweze
kuwakabidhini kwa Halmashauri ili Mkaanze utaratibu wa uchunguzi,” Alisisitiza.
Mmoja wa Watendaji hao Lusilus Bruno wa Kata ya Kirando,
Wilayani Nkasi alikiri kuwepo kwa makosa ya kufanya matumizi kabla ya fedha
hizo kufikishwa kwenye halmashauri jambo linalokwamisha kupokelewa kwa fedha
pungufu wakati wa kuzipeleka benki na kusema kuwa upungufu huo unatokana na
matumizi wanayoyafanya katika shughuli za kila siku za vijiji na kata.
“ Mtendaji wangu wa kijiji Tarehe 15 alinikabidhi shilingi 439,500/=
ambazo tulitoa matumizi ya shilingi 150,000/= ambayo tuliandika dokezo kama
kawaida na kumpa Mkurugenzi akakataa na kusema kuwa matumizi hayo ni makubwa,
hilo deni likafika shilingi 540,100 kwa maana kwamba ile bili ilikuwa bado
inasubiri ile 150,000 ili iende benki lakini mpaka jana ilikuwa bado makusanyo
ni shilingi 100,800/= ambazo alinikabidhi kwahiyo tulishindwa kusafisha bili
kwasababu ya upungufu wa shilingi 150,000,” Alisema.
Kati ya hao waliokabidhiwa TAKUKURU watumishi 22 ni watendaji wa
kata na vijiji kutoka Halmashauri ya wilaya ya Nkasi, na watumishi 18 ni
watendaji wa kata na vijiji kutoka Halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga na mmoja
ni mweka hazina na mhasibu wote wa Wilaya ya Nkasi na wengine 16 kutoka
halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga walitakiwa kuandika maelezo pamoja na
kuambatanisha vielelezo vya kuwasilisha fedha zao kwa mweka hazina wa
halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga.
Comments
Post a Comment