Lugola atoa siku 7 Kuhakikisha Wabakaji Wote Waliokimbilia Zambia Kukamatwa



Waziri wa mambo ya ndani ya nchi Kangi Lugola ameliagiza jeshi la polisi mkoani  Rukwa kuwasaka,kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wabakaji wanne wanaodaiwa kutenda kosa hilo kwa wanafunzi wa shule kisha kukimbilia nchi jirani ya Zambia na kutoa siku saba agizo hilo liwe limetekelezwa.

Ameyasema  hayo kupitia  mkutano wa hadhara uliofanyika katika  kata  ya  Matai Wilayani  Kalambo  mkoani Rukwa, ambapo amesema jeshi la Polisi  liko  imara  na linafanya kazi usiku na mchana hivyo haliwezi kushindwa kuwakamata  wabakaji wanaokimbilia kwenye nchi jirani ya Zambia  na kokote kule baada ya  kufanya  uhalifu.
‘’Watoto hawa lazima walindwe, wabakaji hawawezi kulishinda jeshi la Polisi. Natoa siku saba wote wawe wameishakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria na taarifa hiyo niipate haraka.’’Amesema lugola huku akishangiliwa na mamia ya wananchi.
Aidha, amewataka maredeva wa magari na bodaboda kufuata sheria za usalama barabarani hususani wakati wa kuendesha vyombo vya moto. Vinginevyo watachukuliwa hatua za kisheria ikiwa pamoja na kunyang’anywa leseni.

Wananchi kwa upande wao, wameiomba serikali kufungua kituo cha zima moto kwa lengo la kurahisha upatikanaji wa huduma hiyo pindi majanga ya moto yanapotokea. Hivi sasa huduma hiyo inapatikana Manispaa ya Sumbawanga umbali takribani kilometa 52, kutoka Mji wa Matai ambao ndio makao makuu ya Wilaya ya Kalambo.
Aidha  wamempongeza  mkuu  wa  wilaya  ya kalambo Julieth  Binyura  pamoja  na uongozi wa Halmashauri hiyo kwa kusimamia shuguli mbalimbali za maendeleo  ikiwemo  ujenzi  wa vituo  vya  afya pamoja  na  hospital ya wilaya.


‘’kusema kweli mmetuletea mkuu wa wilaya ambae ni mchapa kazi kwani japo kuwa ni mama lakini anachapa kazi kama mwanaume’’walisema wananchi hao.


Comments