Watano Wafikishwa Mahakamani Kwa Tuhuma Za Uhujumu Uchumi.




Na Ezekiel Kamanga. Mbeya .

Watu watano mkoani Mbeya akiwemo Mfanyabiashara ya madini wilayani Chunya Sauli Mwalabila wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za uhujumu uchumi katika shughuli za madini. 

Pia mshtakiwa wa pili Sauli Samson amechukuliwa na jeshi la polisi mkoani Mbeya baada ya mahakama ya hakimu mkazi Mbeya kukubali maombi ya serikali kumchukua mtu huyo kwa mahojiano juu ya kesi ya uhujumu uchumi anayoshtakiwa nayo pamoja na wenzake wanne mkoani humo.

Mwendesha mashtaka wa serikali wakili mwandamizi Basilius Namkambe akisoma shkata hilo la uhujumu uchumi namba 23/2019 amewataja washtakiwa kuwa ni Micky Konga (53) mkazi wa majengo Itewe na mwenzake Sauli Solomon Mwalabila (39) mkazi wa kiwanja wilayani Chunya.

Amesema wawili hao wanashtakiwa kwa makosa mawili ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kinyume na kifungu namba 302 na 337 ambapo kati ya juni mosi 2019 na Julai 30, 2019 jijini Mbeya walijipatia dola za kimarekani laki moja na 15 kwa ajili ya ununuzi wa madini aina ya dhahabu kutoka kwa raia wa kigeni kutoka nchini Ujerumani Henry Clemar kiasi cha kilo moja wakati sio sahihi kosa la pili likiwa ni uhujumu uchumi kinyume na kifungu namba 12 (b) na 13 (a).

Baada ya Jamuhuri kueleza hayo wakili wa upande wa utetezi Baraka Mbwilo aliitaka mahakama kuzuia mteja wake kutochukuliwa na maaskari hao akisema tangu mfanyabiashara huyo akamatwe sept.mosi mwaka huu alikuwa mikononi mwa polisi waliomsafirisha hadi Dar es Salaam hadi jumatatu hii laasivyo wakaombe magereza kuendelea na uchunguzi wao na kuiomba mahakama iruhusu gari la mshtakiwa lirejeshwe kwa ndugu zake akidai haihusiani na kesi hiyo.

Akijibu hoja hiyo ya utetezi wakili Namkambe wa serikali amesema gari hilo haliwezi kuruhusiwa kwakuwa ni sehemu ya ushahidi maombi na ambayo yameungwa mkono na mahakama kupitia hakimu Denis Luwungo hata kuamuru baada ya kesi hiyo mshtakiwa achukuliwe na jeshi la polisi kwa upelelezi zaidi juu ya shauri hilo.

Pia washtakiwa hao mwingine Emmanuel Kessy Joachim (35) mkazi wa Uyole Mbeya wamefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi Mbeya Andrew Scout na kusomewa pia mashtaka mengine mawili ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji fedha kutoka kwa Sevia Matope raia wa nchini Zambia kiasi cha kwacha 290.

Pia washtakiwa wengine wawili Eveline Bahati (22) mfanyabiashara na na Tyson Jeremia (25) mkulima wote wakazi wa kibaoni chukaa wilayani Chunya wamefikishwa mahakamani Mbeya wakituhumiwa kwa makosa matatu ya kupanga uhalifu, kupatikana na madini sanjari na utakatidhaji wa fedha kosa walilolifanya katika tarehe tofauti kati ya Juni mosi na Agosti 30 mwaka huu huko wilayani Chunya ambapo baada ya kusomewa mashtaka hayo hakimu mkazi katika mahakama ya hakimu mkazi Mbeya Happines Albert Chua ameahirisha shtaka hilo namba 25 la mwaka 2019 hadi Septemba 23 mwaka huu.

Katika kesi na makosa hayo yote washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kutokana mahakama hizo kutokuwa na mamlaka kisheria kusikiliza mashauri hayo ya uhujumu uchumi isipokuwa mahakama kuu ya Tanzania au mahakama ya chini kwa kibali cha mahakama kuu.

Naibu waziri wa madini yupo mkoani Mbeya kwa ziara ya kikazi anasema serikali haitamfumbia macho mchimbaji au mfanyabiashara wa madini atakayekuwa akifanya shughuli hizo kinyume cha sheria ya madini na kuiingizia hasara serikali ambayo inajitahidi kujenga masoko ya madini ili kuisaidia jamii nzima ya watanzania.


Comments