Na Baraka Lusajo. Rukwa.
Mkuu wa mkoa wa Rukwa
Mh.Joachim NWangabo amesifu juhudi za Rais Dkt.John Pombe Magufuli kuhakikisha
anatekeleza ahadi zake alizoahidi kipindi cha kampeni baada ya kutembelea
barabara zinazoendelea kujengwa katika maeneo tofauti ya mkoa huo ikiwemo Kalambo
na Nkasi.
Awali akikagua utekelezaji
wa ujenzi wa barabara ya lami katika miji wa Namanyere wilayani Nkasi mkuu wa mkoa
huo Joachim Wangabo , amesema ahadi ya mheshimiwa rais ni kujenga
barabara zenye jumla ya kilometa tano katika mji na mpaka kufikia mwezi Disemba
mwaka 2019 zitakuwa zimefikia jumla ya kilometa 3.95 ambayo ni sawa na asilimia
79 ya utekelezaji wa ahadi zake na hivyo kumtaka mkandarasi nayeendelea na
ujenzi wa barabara ya kilometa moja afanye haraka kumalizia ujenzi huo ili
wananchi waweze kutumia barabara ambazo zimefungwa kwa muda wa mwaka ili
kupisha ujenzi.
“Huyu mkandarasi
anayejenga kilometa moja kwa kiwango cha lami kazi yake inasuasua kwasababu
mradi huu ulipaswa kukamilika mwezi wa sita mwaka huu na sasa ni mwezi wa tisa,
kazi haijakamilika lakini pia kuna kero ambazo zipo ndani ya barabara hizi,
kuna vivuko vimewekwa vya muda na kwengine hakuna, watu wanapata shida kuvuka
mitaro kwenda kufanya biashara zao lakini pia kwenye matolea ya barabara kuna
vifusi, hivyo nakupa siku 12 utoe vifusi na ujenge vivuko kwenye mitaro,”
Alisisitiza.
Awali akitoa taarifa ya
utekelezaji wa ujenzi wa barabara hizo ili kutimiza ahadi za Mheshimiwa Rais
Mratibu wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijiji Tanzania (TARURA) Mkoa wa
Rukwa Mhandisi Boniface William ,alisema kuwa mbali na kujitahidi kuhakikisha
barabara hizo zinajengwa kwa wakati lakini kumekuwa na changamoto ya ufinyu wa
bajeti pamoja na upatikanaji wa malighafi za ujenzi wa barabara hizo hasa
kokoto.
“katika utekelezaji wa
hii miradi kumekuwa na changamoto mbalimbali, changamoto mojawapo ni ufinyu wa
bajeti, fedha tunayotengewa kulingana na hali halisi ya ‘site’ unakuta ile fedha
ni kidogo kiasi kwamba kama ile barabara ya salala ilikuwa tutengeneze kilometa
moja lakini kwa milioni 350 tulishindwa kutengeneza kilometa moja kwahiyo
tukaweza kutengeneza mita 700 pekee, tatizo jingine ni malighafi kwa maana ya
kuwa na chanzo kimoja cha kokoto katika mkoa, hii inachelewesha kazi,” Alisema.
Katika hatua nyingine,
Mh. Wangabo wakati alipomaliza kutrembelea barabara zenye jumla ya kilometa
moja katika manispaa ya Sumbawanga amewataka wakandarasi wazawa wanaopewa kazi
za ujenzi na TARURA kuhakikisha wanaheshimu na kuzingatia masharti ya mikataba
ili kufanya kazi kwa wakati na kuongeza kuwa ikiwa wakandarasi hao
hawataonyesha uaminifu katika kazi hizo ndogo itakuwa vigumu kwao kupewa miradi
mingine mikubwa.
Katika mwaka wa fedha wa
2019/2020 Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Nkasi
wametengewa bajeti ya shilingi milioni 500 wakati TARURA upande wa Manispaa ya
Sumbawanga wametengewa bajeti ya shilingi milioni 460 ili kuendelea kukamilisha
ujenzi wa barabara katika kutimiza ahadi za Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Comments
Post a Comment