Mapato Ya Halmashauri Ya Kalambo Yaongezeka . Madiwani Wafunguka Siri Ya Mafanikio



Na Baraka  Lusajo. Kalambo.

Halmashauri ya wilaya ya kalambo mkoani Rukwa imefanikiwa kuongeza kiwango cha ukusanyaji wa mapato ya serikali kutoka zaidi ya shilingi milioni mia nane kwa mwaka wa fedha 2017/18 hadi zaidi ya shs bilioni moja kwa mwaka wa fedha 2018/19 kutokana na kuziba mianya ya matumizi yasiyokuwa sahihi ya fedha.

Kaimu mweka hazina wa Halmashauri ya wilaya ya Kalambo,Agustino Manda amewaeleza wajumbe wa kikao maalumu cha baraza la madiwani wa Halmashauri hiyo kilichoketi kuridhia mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha ulioishia june 30 kuwa uadilifu mahali pa kazi umewezesha mafanikio hayo.

Aidha ameelezea jinsi watumishi wa umma katika Halmashauri hiyo walivyozingatia njia sahihi za mapato na matumizi kwa mujibu wa sheria  na kwa kuzingatia nidhamu ya matumizi bora ya fedha za serikali ‘’Financial memorandum of 2017.’’
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo, Daudi Sichone, amesema ushirikiano wa pamoja kati ya wataalamu na viongozi wa kisiasa kwa maana ya madiwani umewezesha kuongezeka kwa mapato ya Halmashauri kunakozingatia kanuni taratibu na sheria ya fedha.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo, Ephraim Mozes   pamoja  na baadhi  ya madiwani  Wilayani  humo  hawakusita  kuelezea mikakati ya  Halmashauri  hiyo katika  swala  zima  la  ukusanyaji  mapato na kusema.

‘’tumenzisha oparesheni ya kukagua magari nyakati za usiku hususani yale ambayo yanahusika na ubebaji  wa mazao ya nafaka  kwani  baadhi  ya  madereva  wamekuwa  wakitorosha mizigo bila  kulipa  ushuru’’ walisema viongozi  hao.

Imeelezwa kuwa mikakati bora ya usimamaizi wa mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo umewezesha kuongezeka asilimia ya ukusanyaji kutoka asilimia 47 hadi kufikia asilimia 61 na hivyo kuwa na uwezo wa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Comments